Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 29Article 560356

Soccer News of Wednesday, 29 September 2021

Chanzo: Mwanaspoti

Bima za wachezaji fupa gumu kwa klabu

Gerald Mdamu, Mchezaji wa Polisi aliepata ajali akiwa na kikosi cha Polisi Gerald Mdamu, Mchezaji wa Polisi aliepata ajali akiwa na kikosi cha Polisi

Mwaka 2012, aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Sepp Blatter aliweka msisitizo kwa wachezaji wote kupatiwa bima za afya wanapocheza mechi zote za kimataifa.

Wakati huo Blatter aliwaeleza wajumbe wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa), kwamba vyama vya soka kote duniani vitatia saini makubaliano hayo hadi kufikia Mei, mwaka huo.

Wachezaji ambao walielezwa kuwa watanufaika na mpango huo ni wale wote waliochezea timu za taifa na klabu kwenye mechi ambazo zinatambuliwa na Fifa.

Itakumbukwa kwamba matukio ya wachezaji kuumia uwanjani hutokea mara kwa mara na mwaka huo ambao Fifa iliweka msisitizo wa bima ya afya, Fabrice Muamba, aliyekuwa mchezaji wa Bolton Wanderers ya Uingereza alikuwa akiendelea na matibabu ya moyo jijini London baada ya kuzirai uwanjani akiitumikia timu yake dhidi ya Fabrice Muamba.

Daktari wa klabu, Jonatahan Tobin alikaririwa akisema Muamba alikuwa ‘amekata roho’ kwa dakika 78 wakati alipofikishwa hospitalini na kupona kwake ilikuwa ni muujiza.

Juhudi za madaktari ndizo zilizomwokoa - alikuwa na uhakika wa matibabu. Wanamichezo wengi nchini wanakumbana na matukio kama hayo wakiwa kwenye majukumu ya soka.

Wapo wanaotibiwa na kupona, lakini wengine wanapitia changamoto ya kupata matibabu kutokana na kukosa fedha na bima za afya ambazo zingewasaidia kipindi hicho.

Klabu nyingi nchini hazina utaratibu wa kutoa bima za afya kwa wachezaji wake na baadhi zimekiri wazi juu ya hilo, jambo linalowapa wakati mgumu wa matibabu wachezaji.

Japo kanuni za Ligi Kuu Bara katika moja ya vipengele vyake ni kwa klabu kuwakatia bima za afya wachezaji wake, lakini wengi wanaeleza kutopata huduma hiyo kwenye ajira zao.

“Kama kuna klabu haitekelezi hilo inapaswa kuchukuliwa hatua na kuwajibishwa,” anasema ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi (TPBL), Almas Kassongo.

UKWELI UKO HIVI

Asilimia kubwa ya klabu hasa za Ligi Kuu hazitoi huduma hiyo kwa wachezaji na hili linaonekana kutopewa uzito unaohitajika.

Wakizungumza kwa sharti la hifadhi za majina yao, wachezaji wa klabu tofauti wanasema hawajawahi kupata bima za afya kipindi chote cha ajira zao.

“Katika mkataba imeandikwa klabu kunikatia bima ya afya, lakini sijawahi kuipata hata mara moja.

“Ikitokea umeumia ukiwa kwenye majukumu ya timu, basi wakati ule ndipo klabu itakuhudumia na si vinginevyo,” anasema mmoja wa wachezaji wa Yanga.

Mchezaji mwingine wa Biashara United anasema mkataba alioingia na klabu hiyo una kipengele cha matibabu, lakini hakisemi anatakiwa kupata bima ya afya.

Mchezaji wa KMC anasema katika mkataba kuna kipengele cha bima ya afya, lakini hawajawahi kupatiwa huduma hiyo japokuwa hupatiwa matibabu wakiumia kazini.

“Bima ya afya kwenye timu yetu katika mkataba ipo, ila ni kwenye makaratasi kwani kiuhalisia hatupewi, japo tunapoumia ukiwa kwenye majukumu ya timu wanakutibia mpaka unapona kabisa,” anasema.

Japo huduma hiyo ni haki ya wachezaji hao ya msingi na wanao uwezo wa kushtaki kama klabu zinaenda kinyume, wachezaji wengi wanasema wanashindwa kuchukua hatua wakihofia kuharibu ajira zao.

“Hiyo ni kanuni kabisa. Klabu lazima iwape bima ya afya wachezaji wake,” anasema Kassongo.

Anasema upande wao ni wasimamizi tu, lakini klabu zote zinapaswa kuambatanisha kwenye mikataba ya wachezaji na nyaraka za bima za matibabu.

“Sijui utekelezaji ukoje, lakini kimsingi kama klabu haitekelezi hilo basi inapaswa kuchukuliwa hatua,” anasema.

Anasema anayepaswa kuchukua hatua ni mchezaji ambaye ndiye mwajiriwa dhidi ya mwajiri wake.

“Anaweza kumshtaki mahakamani au TFF, inategemea suala hilo liko katika muktadha upi kwani kama klabu haitoi bima ya afya na wakati mnaingia mkataba mlikubaliana hilo ni kosa.

“Mchezaji ni haki yake kupewa bima na kuhoji endapo klabu haitekelezi hilo, kwa kuwa bima ya afya iko kwenye kanuni, hivyo ni wajibu wao kuidai na si kusubiri hadi uumie.”

KLABU HIZI HAPA

Yanga ni miongoni mwa klabu ambazo hazina utaratibu wa kuwapa bima za afya wachezaji wake.

Aliyekuwa katibu mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa anakiri klabu yao kutokuwa na huduma hiyo kwa wachezaji, ingawa anasisitiza kuwa inatambua umuhimu wa kutoa huduma hiyo kwa wachezaji.

“Tuko mbioni kuanza kuitoa. Tumeshafanya mazungumzo na watu wa bima ya afya ambao wana utaratibu wa kutoa nafasi kwa wanamichezo,” anasema Mfikirwa.

“Hivyo klabu yetu pia itaingia kwenye utaratibu huo na utakapokamilika wachezaji wetu wataanza kuingia kwenye mfumo wa NHIF.”

Mtendaji mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakari anasema wachezaji ni sawa na watumishi wengine wa kampuni, hivyo kila anayeingia ndani lazima awe na bima ya afya.

“Wachezaji nao ni watumishi pia wa kampuni. Kwa hiyo bima lazima wawe nayo, hao ni wafanyakazi kama walivyo wengine ndani ya taasisi,” anasema Swabri akimaanisha kwamba hata wachezaji hupewa.

Ofisa habari wa Polisi Tanzania, Hasan Juma anasema kuanzia msimu huu kila mfanyakazi wa timu hiyo atakuwa na bima ya afya na hii ni kutokana na funzo walilopata baada ya mchezaji wao, Gerald Mdamu kuumia.

“Yaani hata yule anayekusanya vifaa atakuwa na bima. Ishu ya Mdamu imetufunza vitu vingi sana, hivyo msimu ujao (huu) yeyote anayeitwa mtumishi wa Polisi Tanzania atakuwa na bima,” anasisitiza Juma.

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Biashara United, Hajji Mtete anasema msimu huu bima kwa wachezaji na benchi la ufundi ni lazima na ni kipaumbele chao.

“Ni mara ya kwanza kuwa na ishu hii muhimu, kila mchezaji na benchi la ufundi wote watakuwa na bima za afya, hili ni suala nyeti sana na tunalipa kipaumbele,” anasema Mtete bila kueleza walipofikia katika utekelezaji wake.

Katibu mkuu wa Tanzania Prisons, Ali Mrisho anasema kwa wachezaji ambao ni askari wana bima za afya, huku wale wengine yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kuwa wanakuwa nazo.

“Kwa upande wa wachezaji ambao ni askari wote wana bima za afya, ila nipo kwenye mchakato kulifanyia kazi kwa hawa wengine ambao ni raia wa kawaida,” anasema Mrisho.

Naye mwenyekiti wa Mbeya Kwanza, Mohamed Mashango anasema bima za afya ni muhimu na ni kanuni kwa maelezo ya TFF, hivyo wanalipa kipaumbele suala hilo. “Sisi hiyo ni lazima na muhimu. Kwanza kanuni zinaelekeza hivyo. Kwa hiyo kila mchezaji wetu ana bima ya afya tuko makini sana kwenye hilo,” anasema Mashango.

Dodoma Jiji FC kupitia kwa katibu mkuu, Fortunatus Johnson anasema tayari wameshatenga bajeti kuhakikisha kila mchezaji na benchi la ufundi wanakuwa na bima za afya.

“Tumeshatenga bajeti na sasa tupo kwenye utekelezaji, hivyo msimu ujao lazima kila mmoja ndani ya timu awe na bima ya afya. Ni muhimu sana hii huduma,” anasema Johnson.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa Kagera Sugar, Masoud Ally anasema kama ilivyokuwa msimu uliopita bado hakuna mabadiliko na msimu huu lazima bima za afya kwa wachezaji na benchi la ufundi.

“Hapana. Bima ni muhimu sana. Hakuna mabadiliko kila mchezaji au kocha lazima wawe nayo. Lazima tujali afya za kila mfanyakazi wetu,” anasema.

Kwa upande Namungo wanasema ni kipaumbele msimu huu kwa wachezaji wote kuwa na bima za afya na hiyo ni kutokana na kazi wanayoifanya wawapo uwanjani.

“Ni kipaumbele kikubwa sana kwetu na msimu ujao (huu) tunaamini kila mchezaji atakuwa na bima ya afya. Tayari tumetenga bajeti na tupo kwenye utekelezaji,” anasema Ally Suleiman, katibu mkuu wa klabu hiyo.

NHIF WAVUNJA UKIMYA

Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya (N-HIF), Bernard Konga anasema mwanasoka kuwa na bima ya afya ni sawa muhimu kama ilivyo mtu mwingine yeyote.

“Klabu hazina mwamko kwenye hili. Wengine wanapoumwa ndipo wanakumbuka umuhimu wa bima ya afya, lakini wakati huo na sisi hatuwezi kukupa,” anasema.

Konga anasema bima ya afya ni muhimu kwa kila mmoja, japokuwa klabu kutoingia huko ni wao wenyewe kukosa mwamko.

“NHIF tumeunda utaratibu kwa wanamichezo kupata bima za afya kupitia klabu zao, lakini sijaona timu kuwa na mwamko.”

Mkurugenzi huyo anasema msimu huu wamezungumza na TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa klabu kuwa na utaratibu huo, hivyo ni uamuzi wa klabu na mtu binafsi kupata bima.

“Isije kutokea baadaye umeumwa na umeshindwa kupata matibabu ndipo unaanza kulaumu au unakumbuka kutafuta bima ambayo kiuhalisia hatuwezi kukupa kwa wakati huo.

“Hivyo ni wajibu wa wachezaji wenyewe kuona umuhimu wa bima za afya kwani hizo ni mtaji wao katika afya zao,” anasema.

Mkakati huo wa NHIF unakuja ikiwa ni miaka sita imepita tangu ilipoingia makubaliano ya mwaka mmoja na TFF kutoa bima za afya kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kwa klabu 16 vya Ligi Kuu Bara 2015.

Aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine anasema utaratibu huo utazisaidia klabu za Ligi Kuu katika matibabu ya wachezaji na bechi ka ufundi na kuondoa kilio cha muda mrefu kwenye matibabu ambayo ni suala la kikanuni ingawa klabu zimeshindwa kutimiza hitaji hilo.

SPUTANZA YAONYA

Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (Sputanza), Mussa Kisoki anasema msimu huu hawataruhusu mchezaji kupewa leseni ya kucheza bila kuwa na bima za afya.

“Hatutakuwa na mzaha katika hili, tumezungumza na TFF kukamilisha hili kwa kila mchezaji mwenye bima ya afya ndiye atapatiwa leseni,” anasema Kisoki.