Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 28Article 554095

Soccer News of Saturday, 28 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Bocco hatihati kuivaa DR Congo

Mshambuliaji wa Taifa Stars, John Bocco Mshambuliaji wa Taifa Stars, John Bocco

Mshambuliaji wa Taifa Stars, John Bocco huenda akaikosa mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 dhidi ya DR Congo unaotarajia kuchezwa Septemba 2, mjini Lubumbashi.

Taifa Stars imeanza kambi kwa siku ya tatu sasa kujiandaa na mechi hiyo bila mchezaji huyo kufanya mazoezi na wenzake kutokana na majeraha ya mguu yanayomkabili.

Meneja wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema bado ni mapema kufahamu kama mchezaji huyo atakuwa miongoni mwa watakaocheza mechi hiyo au vinginevyo kutokana na kutogusa uwanjani kabisa.

“Bocco yupo kambini lakini hajaweza kufanya mazoezi na wenzake tangu kambi imeanza, hivyo hatma yake kucheza au vinginevyo daktari wa timu atatoa muongozo, ila kwa sasa ni mapema kusema kama atacheza mechi hiyo au la,” amesema Cannavaro.

Meneja huyo amesema wachezaji wengine wanaendelea na mazoezi vizuri kwenye kambi yao yenye wachezaji 25.

Taifa Stars itacheza na DR Congo Septemba 2 , baadaye itacheza na Madagascar Septemba 7, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.