Uko hapa: NyumbaniMichezo2022 01 10Article 584746

Soccer News of Monday, 10 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Bwalya: Tunazidi Kuingia Kwenye Mfumo wa Kocha

Bwalya Bwalya

RALLY Bwalya, kiungo wa Klabu ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco amesema kuwa bado wanaendelea kuingia kwenye mfumo wa kocha huyo ambaye anawasisitizia wapambane kupata matokeo.

Pablo alibeba mikoba ya Didier Gomes ambaye alibwaga manyanga kutokana na timu hiyo kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sasa ana kazi ya kupambania Kombe la Mapinduzi lililo mikononi mwa Yanga.

Bwalya mkononi ana tuzo ya mchezaji bora wa mchezo ambayo aliipata kwenye mchezo dhidi ya Selem View uliochezwa Uwanja wa Amaan wakati Simba ikishinda kwa mabao 2-0.

Nyota huyo alisema: “Kikubwa ambacho tunakifanya ni kuona kwamba tunapata matokeo na tunazidi kuona namna gani tunaweza kwenda na mfumo wa mwalimu ambaye anatufundisha na amekuwa akituambia kwamba tunapaswa kushinda mechi zetu ambazo tunacheza.”

Simba imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na inatarajiwa kucheza na Namungo.