Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 18Article 572416

Soccer News of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: Mwanaspoti

CV ya De Castro wa Simba hatari tupu

De Castro De Castro

UJIO wa Kocha mpya wa viungo wa Simba, Don Daniel De Castro sio habari kubwa sana mjini kama ilivyokuwa kwa kocha mkuu Pablo Franco, ila kwa wasifu ni wazi Wekundu wa Msimbazi wamelamba dume.

Castro ambaye amekuja kuziba nafasi ya Adel Zrane raia wa Tunisia aliyeachana naye hivi karibuni, ana digrii ya Physical Fitness Training aliyoipata Chuo cha Real Madrid na amewahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya vijana chini ya miaka 18 ya Real Madrid msimu wa 2018/19.

Costro alihusika kuwatengeneza nyota kama Carlos Algarra anayechezea Cadiz, Sergio Lopez aliyepo FC Basel, Cesar Gelabert anayeitumikia Milandes na Fran Garcia aliyepo Rayo Vallecano.

Msimu wa 2019/20, alikuwa kocha msaidizi wa viungo wa timu ya Rapid Bucharest ya Romania na 2020/21 alikuwa kocha msaidizi wa viungo wa Politehnica Ias ya Romania.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema walitoa nafasi ya makocha kutuma maombi na CV iliyoangaliwa na kupitishwa ni ya kocha huyo kwani walivutiwa nayo.

“Suala la mkataba wa muda gani hilo ni baina yetu na mwajiriwa, kuhusu kocha huyo kupendekezwa na Pablo hapana, ni maombi yalitolewa na tumemchukua kutokana na kuwa na wasifu mzuri,” alisema Mangungu.

Kocha huyo aliwasili jijini Dar es Salaam mapema juzi na jana alianza kazi akiungana na Pablo aliyejiunga na timu hiyo wiki iliyopita.