Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 16Article 551785

Soccer News of Monday, 16 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

"Chama alilazimisha kuondoka Simba" - Magori

Aliyekua Kiungo wa Simba SC, Clatous Chama ambae katimkia nchini Morocco Aliyekua Kiungo wa Simba SC, Clatous Chama ambae katimkia nchini Morocco

Mshauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba Crescentius Magori amesema suala la kuondoka kwa kiungo wao Clatous Chama  lilikuwa ni jambo la kushtua kwa sababu  hawakuwa na mpango wa kumwachia mchezaji huyo.

Magori amesema nayo wakati anahojiwa kwenye kituo cha radio cha EFM kuwa kama Chama asingeondoka walitaka kumpa mkataba mpya utakaomfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi kuliko wachezaji wote wa Tanzania ila baada ya kuja ofa nzuri wakaona ni vyema kumruhusu kuondoka

"Chama aliweka msukumo mwenyewe wa kutaka kuondoka, lakini mwekezaji wetu Mohamed Dewji 'Mo' alikataa lakini baadae alikubali," amesema Magori.

Ameongeza kuwa "Tumefanya ujasusi wa mpira na kugundua kuwa mkataba tuliokuwa tunataka kumpa Chama ungemfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi nchini lakini baada ya kuona kuwa huko anakoenda atalipwa mshahara mara tatu zaidi kuliko Simba tukaona ni busara kumuachia," alisema.

Magori alisema kuwa Chama aliomba kuondoka mwenyewe akisema kuwa hajawahi kucheza timu moja kwa misimu mitatu mfululizo, licha ya kocha Didier Gomes na mwekezaji "Mo" kutokubaliana na suala hilo hapa awali.

"Chama alisema kuwa amekaa hapa kwa miaka mitatu amepata kila kitu kuanzia Ligi kuu, ameipeleka timu hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), umri wake umekwenda hivyo sisi kama viongozi tukakaa na kuona bora tumuachie kwa sababu ametusaidia sana hivyo tumuache akapate changamoto sehemu nyingine," amesema

Kuhusu mbadala wa Chama Magori amesema kuwa ni ngumu sana kwa sababu unapaswa kutumia vigezo vingi ili kuhakikisha anasaidia kwa kiasi kikubwa.

"Unapomtafuta mbadala wa Luis na Chama lazima usingatie vitu vingi sana lakini sio kuleta mchezaji ambaye lazima afanane na aliyeondoka ila kuleta mchezaji ambaye ataingia kwenye timu kutokana na mapendekezo ya mwalimu," amesema.

Magori pia amezungumzia ishu ya Luis Miquissone aliyejiunga na mabingwa wa Afrika Al Ahly ya Misri kuwa ni pigo kwa timu hiyo lakini wasingeweza kumzuia kutokana na fedha iliyowekwa.

Magori amesema kuwa suala la kumuuza mchezaji huyo wameangalia zaidi kipaji chake kwa sababu anaenda timu kubwa na wao kama uongozi walijua ataondoka hivyo wakaanza kujipanga mapema kwa ajili ya kutafuta mbadala wake.

"Watu wamekuwa na malalamiko kuhusu kuondoka kwa Luis lakini fedha iliyowekwa ni kubwa zaidi kuliko hata wachezaji wa Ulaya maana anakwenda kulipwa mara nane zaidi ya alivyokuwa analipwa Simba," amesema Magori.

Wachezaji waliosajiliwa na Simba mpaka sasa ni Yusuph Mhilu, Hennock Inonga 'Varane', Pape Ousmane Sakho, Duncan Nyoni 'Monster', Peter Banda, Saido Kanoute, Jimson Mwanuke, Abdulswamad Kassim, Kibu Denis, Jeremia Kisubi na Israel Patrick.