Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 29Article 560248

Soccer News of Wednesday, 29 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Changamoto nne za Gomes Simba, nani wa kumsaidia?

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes

Ni kama mtumbwi uliokumbwa na dhoruba kali katika Bahari ya Shamu, ama mvua kali wakati wa mavuno, ndivyo hali ilivyo kwa kocha Didier Gomes pale Simba. Mambo yamemwangukia.

Simba imecheza michezo mitatu sasa bila kufunga goli. Miwili kati ya hiyo ni ya mashindano. Haijawahi kutokea ndani ya muda mrefu. Simba ndio wababe wa soka la Tanzania kwa sasa. Inawezaje kucheza mechi tatu bila kufunga goli? Inafikirisha sana.

Hata hivyo, kuna changamoto nne zinazomkabili kocha huyo mtaalam wa mpira pale Simba.

1. Kuziba pengo la Chama na Miquissone.

Hakuna kazi nyepesi kama kufundisha timu yenye Chama na Miquissone. Utafanya kazi yako kiasi wao wataimalizia. Hata makocha wa Mchongo kama Ahmed Ally na Kassim Liogope wangeweza kuipa matokeo timu yenye Chama na Miquissone. Nini kinafuata baada ya nyota hao kuondoka? Hapa ndipo kazi ya kocha inapoanza. Gomes ana kazi kubwa ya kuziba pengo la mafundi hao pale Msimbazi. Utaalam na mbinu zake ndio zitaifanya Simba ifanye vizuri bila ya wawili hao.

2. Kupata ubora wa nyota wake

Wachezaji wengi wa Simba wamechoka. Wamecheza kwenye ubora wa juu kwa miaka minne mfululizo. Ni ngumu kuupata ubora wao kirahisi tena. Ukiwatazama Tshabalala na Kapombe wamechoka. Bocco amechoka. Hapo Gomes anatakiwa kuwa na program nzuri ya kuwafanya waendelee kucheza katika ubora wao.

3. Namna ya kuwatumia nyota wapya

Simba imesajili nyota 12 wapya. Ni ajabu na kweli. Timu iliyotoka kufika robo fainali CAF na kubeba makombe yote ya Ndani ilihitaji usajili wote huu? Sasa kazi ipo kwa Gomes kuhakikisha nyota hao wanafanya vizuri. Banda, Sakho, Nyoni wa Malawi, Mwanuke na wengineo. Anahitaji kuwatumia vizuri.

4. Simba icheze pira Biriani

Hata kama Simba itaanza kushinda mechi zake, mashabiki na viongozi wa Simba siku zote wanataka timu yao icheze Pira Biriani. Yaani pasi 800 halafu linafungwa goli tamu. Ikishindikana hapo ni ngumu kumuelewa kocha wao. Hiki kimewafukuzisha makocha wengi Msimbazi akiwemo Patrick Aussems.