Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 23Article 559216

Soccer News of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Coastal Union yaitumia salamu Azam FC

Wagosi wa Ndima, Coastal Union kutoka Jijini Tanga Wagosi wa Ndima, Coastal Union kutoka Jijini Tanga

Coastal Union imesema ile desturi yao ya kutumia vyema uwanja wa nyumbani itatumika vizuri katika mchezo wao wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC kwa kuhakikisha inapata pointi tatu.

Timu hiyo itaikaribisha Azam FC katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga Septemba 27, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Coastal Union, Jonathan Tito, amesema kikosi hicho kinaendelea na maandalizi mazuri kuhakikisha kinaanza vizuri ligi hiyo.

“Timu inaendelea vizuri na mazoezi na sasa tunatazama mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Azam FC utakaochezwa wiki ijayo, kocha anakiandaa kikosi kucheza kwa ushindi kusudi kipate matokeo mazuri ya kuanzia,” amesema.

Tito amesema kwa namna walivyojipanga hawataki kurudia makosa ya msimu uliopita kufanya vibaya na wamejipanga kushinda dhidi ya yeyote watakayekutana naye.

Kwa mujibu wa Tito, Kocha wa Coastal Union, Melis Medo raia wa Marekani pamoja na wachezaji wameweka malengo ya kuhakikisha wanafanya vizuri msimu ujao ikiwezekana kuingia katika nne bora za juu.

Timu hiyo ilinusurika kushuka daraja msimu uliopita na kilichowaokoa ni mchezo wa mtoano wa kupanda au kushuka ambao walivuka salama dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza la Pamba na kubaki Ligi Kuu.

Ili kutorudia makosa ya msimu uliopita, Coastal iliamua kumwajiri kocha huyo mgeni kutengeneza kikosi upya ili kurudi katika ushindani msimu huu.