Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 21Article 552817

Soccer News of Saturday, 21 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Diarra afanya balaa langoni

Golikipa wa Yanga, Diarra Djigui Golikipa wa Yanga, Diarra Djigui

Kipa mpya wa Yanga, Diarra Djigui ameonyesha uhodari mkubwa mazoezini kwa hesabu zake hatari akiwa langoni.

Jana Diara amewashtua hata wachezaji wenzake ikiwemo kuwa na uamuzi wa haraka langoni huku hesabu zake nyingi zikienda sawa ikiwa ni mazoezi yake ya kwanza tu ya kucheza.

Kipa huyo wa timu ya taifa wa Mali, jana aliwakosha waliomshuhudia kutokana na wepesi wake katika kuruka na kudaka mipira kwa umakini mkubwa.

Uimara wa Diarra jana ulimfanya mshambuliaji Ditram Nchimbi kujikuta anashindwa kujizuia akikubali kazi yake kwa nguvu akisema; “Hili kipa hili kazi tunayo,” kauli hiyo iliwachekesha mabosi wengi ambao walikuwa nje wanafuatilia mazoezi hayo.

Hata hivyo, alikuwa ni mshambuliaji Fiston Mayele pekee aliyetibua rekodi ya kipa huyo akimfunga bao moja.

Mbali na Diarra, kipa mzawa Erick Johola naye sio kipa wa mchezo, kwani jamaa alionyesha uhodari wa kudaka mashuti makali hasa ya juu ambapo jana tu aliokoa mashuti manne makali ambayo kama sio umakini wake yalikuwa yanaingia ndani ya nyavu.

Yanga jana imefanya mazoezi ya kwanza ya kucheza soka wakigawanya wachezaji katika makundi mawili katika nusu uwanja ambapo wachezaji walionekana kuchangamka wakionyesha ufundi wao.