Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 18Article 572602

Soccer News of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Gadiel Michael: Tunaiheshimu Ruvu Shooting

Gadiel Michael Gadiel Michael

Beki wa Kushoto wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Gadiel Michael amesema kikosi cha klabu hiyo kimejipanga kushinda mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting kesho Ijumaa (Novemba 19).

Simba SC itakua mgeni katika mchezo huo utakaounguruma Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, na tayari kikosi cha Mabingwa hao watetezi kimeshawasili jijini humo tangu jana Jumatano (Novemba 17).

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Alhamis (Novemba 18) majira ya mchana Jijini Mwanza, Gadiel Michael amesema wamejiandaa kikamilifu kupambana kuelekea mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania.

Amesema licha ya kujiandaa vizuri, bado wanaiheshimu Ruvu Shooting ambayo itakuwa mwenyeji katika mchezo huo, ambao umepangwa kuanza majira ya saa kumi jioni.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini tumejipanga kushinda. Naamini mtaona mabadiliko.” amesema Gadiel Michael.

Simba SC inakwenda kwenye mchezo wa kesho ikiwa na alama 11 zinazoiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Ruvu Shooting ikiwa na alama 6 zinazoiweka nafasi ya 10.

Simba SC ilishinda mchezo wake uliopita dhidi ya Namungo FC kwa bao 1-0, huku Ruvu Shooting ikipoteza mbele ya Young Africans kwa mabao 3-1.