Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 18Article 572548

Soccer News of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Geita Gold, Kagera Sugar watunishiana misuli

Kagera Sugar, Geita Gold tambo kila kona Kagera Sugar, Geita Gold tambo kila kona

Ikiwa zimesalia saa chache kabla ya Kagera Sugar na Geita Gold kuvaana katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, timu hizo zimetambiana kila mmoja akizitaka pointi tatu za mtanange huo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.

Timu hizo zilikutana katika mechi mbili za kirafiki kujiandaa na msimu huu ambapo Geita ilishinda ugenini Kaitaba kwa mabao 2-1 kisha wakatoshana nguvu kwa sare ya 1-1 Nyankumbu kwenye siku maalum ya Geita Gold kutambulisha wachezaji wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nahodha Msaidizi wa Geita, Chilo Mkama amesema maandalizi yao chini ya Felix Minziro yanakwenda vizuri na wamejipanga kuchukua pointi tatu muhimu dhidi ya Kagera mchezo huo utakaopigwa kuanza saa 10:00 jioni.

Beki huyo wa zamani wa Mbao, Toto Africans, Pamba na Kumuyange amesema makosa madogo yaliyojitokeza kwenye mechi zilizopita yamerekebishwa na timu iko tayari kwa kupigania ushindi huku akiamini kocha wao anaweza kuwafikisha pazuri.

“Timu ipo vizuri ni makosa madogo ambayo tumeyatengeneza katika mechi tano za awali Mwalimu aliyaona na kuyafanyia kazi na tumejipanga katika mechi zijazo tutafanya vizuri tukianza na Kager Sugar ugenini,” amesema Mkama.

“Minziro ataisaidia timu inawezekana na vijana anao wa kufanya kazi na ikaenda vizuri kikbwa sisi kama wachezaji tupo tayari kwa kazi kwa manufaa ya timu na maendeleo ya kila mmoja wetu,” amesema.

Kwa upande wa Kagera, Kocha wake Mkenya Francis Baraza amesema baada ya mapumziko ya wiki moja wachezaji walirejea na kuanza mazoezi mepesi ya kurejesha utimamu wa mwili ambapo anawatafutia mechi moja ya kirafiki ili kuwa fiti kabla ya mtanange huo.

“Naushukuru uongozi wa timu mashabiki na benchi la ufundi kuwa pamoja kwasasa timu inaendelea na mazoezi tunafanyia kazi upigaji pasi na mfumo (formation) na vijana wanashika haraka, najaribu kuona kama kesho jioni (Jumatano) tutapata mechi ya kirafiki,” amesema Baraza.

Beki wa timu hiyo, Dickson Mhilu amesema wamejiandaa vizuri na wanauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa wakihitaji pointi tatu ili kuendelea kuwa katika timu za juu kunako msimamo wa ligi hiyo.