Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 25Article 559579

Soccer News of Saturday, 25 September 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Gomes Awapa Sakho, Banda Majukumu

Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Pape Ousmane Sakho Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Pape Ousmane Sakho

Katika kuhakikisha timu yake inapata ushindi kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amewapa majukumu mapya viungo wake wa pembeni.

Viungo hao wa pembeni hivi sasa wanaongozwa na Ousmane Sakho, Peter Banda na Duncan Nyoni ambao wote ni wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo.

Nyota hao wa kigeni wanatarajiwa kuwepo katika orodha ya kikosi cha Gomes kitakachocheza dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kesho Jumamosi saa 11:00 jioni, Uwanja wa Mkapa, Dar.

Mmoja wa mabosi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa tangu timu hiyo imeingia kambini juzi Jumanne, kocha huyo ameonekana akiifanyia maboresho safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Denis Kibu, John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere.

Bosi huyo amesema kuwa katika mazoezi hayo, kocha ameonekana akitaka kufanya mashambulizi kupitia viungo na mabeki wa pembeni kwa kupiga krosi na kona safi kwa washambuliaji wake ili kuhakikisha wanapata nafasi nyingi za kufunga.

Ameongeza kuwa akiendelea na program hiyo, kocha huyo alionekana kuwapa maelekezo viungo hao wa pembeni jinsi ya kupiga krosi nzuri za juu na chini ambazo alitaka zifikie ndani na nje ya 18 huku akiwataka kufunga kwa kichwa, mashuti na kumchambua kipa.

“Kama unakumbuka vizuri Kocha Gomes amekuwa akitumia mbinu mbalimbali za kushambulia na mara nyingi amekuwa akitumia kupitia katikati kwa ajili ya kufunga mabao.

“Lakini katika kuelekea mchezo ujao wa Ngao ya Jamii ameonekana akiwaandaa viungo wake wa pembeni watatu ambao kazi yao wao ni kupiga krosi safi kwa washambuliaji wake akina Kibu, Mugalu, Bocco na Kagere.

“Hiyo ni ishara tosha katika kuelekea mchezo huo anataka kushambulia kwa kupitia pembeni akiwatumia viungo wapya Sakho, Banda na Duncan ambao wameonekana wapo vizuri,” amesema bosi huyo.

Akizungumzia mchezo huo, Gomes alisema: “Malengo ni kuhakikisha tunawafunga Yanga, kwani ushindi huo utakuwa mwanzo mzuri kwetu katika kutetea makombe tunayoyawania msimu ujao.”