Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 24Article 544045

Habari za michezo of Thursday, 24 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Gomes: Mechi na Yanga ngumu

Gomes: Mechi na Yanga ngumu Gomes: Mechi na Yanga ngumu

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wa jadi Yanga utakuwa mgumu, ingawa anaimani kuwa kikosi chake kitaibuka na ushindi.

Amesema katika mchezo huo watacheza kama fainali sababu wanajua wakishinda watakuwa wametetea ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo.

Simba na Yanga zitakutana Julai 3 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa marudiano ambao awali ulipangwa kuchezwa Mei 8, lakini haukufanyika kutokana na mkanganyiko wa muda wa mchezo kubadilishwa dakika za mwishoni kinyume cha kanuni za ligi hiyo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa Simba dhidi ya Mbeya City juzi, ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1, Gomes alisema mechi yao na Yanga itakuwa ngumu mgumu kwa timu zote mbili, lakini ana imani kubwa na ushindi kutokana na ubora wa kikosi chake ikilinganishwa na cha wapinzani wao Yanga.

“Tumebakisha mechi tano na tunahitaji pointi tatu tu tutangazwe mabingwa na mchezo unaofuata ni dhidi ya watani zetu Yanga, najua itakuwa kama fainali, nawaamini wachezaji wangu na tutafanya vizuri na kuibuka washindi,” alisema Gomes.

Endapo Simba itafanikiwa kuifunga Yanga itafikisha pointi 76 ambazo hazitafikiwa na watani zao hao ambao baada ya mchezo huo kama watashinda mechi zote zilizobakia watafikisha pointi 73 ambazo zitakuwa tayari zimepitwa na Wekundu hao wa Msimbazi.

Aidha, Gomes alimpongeza kiungo wake wa kimataifa raia wa Zambia, Cletus Chama kwa kiwango kizuri alichokionesha kwenye mchezo huo ikiwamo bao alilofunga, ambalo alisema litamsaidia kumrudisha mchezoni na kumsahaulisha magumu aliyopitia baada ya kufiwa na mke wake.

“Nimefurahishwa na kiwango alichokionesha ingawa ameripoti juzi (jana) mazoezini akitokea Zambia, lakini amecheza vizuri na tulipanga kumpa dakika 30 kwa ajili ya kumrudisha mchezoni ili kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga awe ni miongoni mwa wachezaji watakaoanza,” alisema Gomes.

Kwa upande wake, Kocha wa Mbeya City, Mathias Lule alikubali matokeo hayo akisema wachezaji wake walizidiwa kimbinu na kushindwa kufuata kwa usahihi maelekezo aliyowapa ndio maana wakapoteza mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao.

Alisema pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini bado hawajakata tamaa ya kuipigania timu hiyo kubaki Ligi Kuu Bara msimu ujao kwani wamejipanga kushinda mechi zote mbili zilizobaki kabla ya msimu kumalizika kwa msimu.