Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 21Article 558868

Habari za michezo of Tuesday, 21 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Gomes: Sikulenga matokeo Mazembe

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes

BAADA ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo kwenye mechi ya kirafiki iliyopigwa katika Tamasha la Simba Day, Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema kuna kitu alichokuwa akihitaji kukiangalia zaidi kikosini kuliko matokeo ya ushindi.

Akizungumza na Nipashe baada ya mchezo huo, Gomes alisema kwa kiasi kikubwa wachezaji wake walifanya kile ambacho amewaelekeza, isipokuwa kuna kasoro chache ambazo sasa anakwenda kuzifanyia kazi kabla ya kukutana na Yanga Jumamosi wiki hii kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii maalum kwa ajili ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2021/22.

“Ulikuwa mchezo mzuri sana kwetu, binafsi sikuwa natafuta zaidi matokeo na badala yake nilichokuwa nakiangalia ni namna wachezaji wanavyoweza kutekeleza kile nilichowafundisha na kwa kiasi kikubwa nimeona juhudi zao.

“Kama uliangalia vizuri ule mchezo tulipoteza nafasi kadhaa nzuri ambazo endapo tungezitumia vizuri, tungeweza kupata ushindi, hivyo tunakwenda kurekebisha haya mapungufu, ili kufanya vizuri zaidi michezo yetu inayokuja,” alisema.

"TP Mazembe walikuwa na kiwango bora kuliko sisi, tukumbuke tuliwahi kucheza nao katika mchezo wa ushindani, safari hii wamerudia tena wakiwa bora zaidi yetu, nadhani hii itatusaidia sana," alisema Gomes.

Gomes alisema mchezo huo utakuwa umewapa somo kubwa wachezaji wake kuelekea mechi dhidi ya Yanga Jumamosi wiki hii huku akidai kuwa, ana imani kubwa na kikosi chake.

Wakati Gomes akisema hayo, Kocha Mkuu wa TP Mazembe, Franck Dumas, alisema: “Tumewafunga lakini haikuwa kazi nyepesi, hawa jamaa ni wapambanaji sana, ndiyo maana katika misimu hii ya hivi karibuni wamekuwa wakipata matokeo mazuri michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika."