Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 22Article 552973

Soccer News of Sunday, 22 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Gomes aitisha kikao fasta

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes

Simba jioni ya jana walikuwa wakitesti mitambo kwa kuvaana na FAR Rabat kama sehemu ya maandalizi yao ya msimu mpya nchini Morocco, lakini mara baada ya mchezo huo Kocha Didier Gomes alipanga kukutana mastaa wake ili kupeana michongo mipya.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Rabat ilipo kambi ya Simba, Gomes amesema kikao hicho kitasaidia kwa wachezaji walioingia na wale waliokuwapo kujua falsafa zake mpya kwa msimu mpya akiwa na kiu ya kuona Simba inafika mbali zaidi ya ilivyokuwa msimu uliopita.

“Wachezaji wapya hawaifahamu vema falsafa ya Simba na kuielewa kiundani timu yao, hivyo baada ya mechi tutakuwa na kikao nao maalumu kuwaeleza kwa kina kuhusu timu hii na mipango yake kabla ya kutafuta mechi nyingine za kirafiki kuendelea kuwasoma vizuri wachezaji wangu,” amesema Gomes.

Juu ya mchezo wao wa jana dhidi ya FAR Rabat inayonolewa na mtangulizi wake Msimbazi, Sven Vandenbroeck uliopigwa saa 10 jioni kwa saa za Morocco sawa na saa 12 za Tanzania, ulikuwa maalum kwake kuanza kuwasoma vijana wake kwa kuwasoma mmoja mmoja.

“Ni mechi muhimu kwetu kila mmoja kupima kiwango chake, lakini pia itatusaidia kuona nini tunapaswa kurekebisha kwenye kikosi chetu, ila mpaka sasa vijana wangu wanazidi kuimarika, na hasa baada ya wachezaji wapya kujumuika pamoja na wenzao,” amesema Gomes aliyedokeza kabla ya kurudi nchini timu yake itacheza pia mechi nyingine mbili japo hakuweza kutaja majina ya timu hizo.