Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 09Article 541681

Habari za michezo of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Gomes kuimarisha kikosi chake

Gomes kuimarisha kikosi chake Gomes kuimarisha kikosi chake

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes ametamba akisema akili yake kwa sasa inawaza namna ya kukiimarisha kikosi chake cha msimu ujao, na siyo mechi zilizosalia sababu haoni kama kuna timu pinzani ambayo itaweza kumsumbua kutetea mataji yao mawili wanayoyashikilia.

Simba ndio vinara wa mbio za kuwania taji la Ligi Kuu hivi sasa wakiwa na pointi 67 katika michezo 27 walizocheza mpaka sasa, huku wakiwa na faida ya michezo miwili mkononi ili kulingana na watani zao Yanga waliopo nafasi ya pili na pointi zao 61.

Akizungumza na gazeti hili Gomes, alisema kwake yeye nikama ameshamaliza msimu na anachokifanya nikufikiria zaidi msimu ujao namna ya kukijenga kikosi chake kwa kuongeza wachezaji, ambao wataifikisha mbali timu hiyo hasa kwenye michuano ya kimataifa.

“Tumebakiwa na michezo saba kabla ya kumaliza msimu kwa ubora tuliokuwa nao hivi sasa ukilinganisha na ule wa wapinzani wetu naona kama ligi imekwisha na Simba ndio bingwa hata kwenye Kombe la FA bado sijaona timu ambayo itatuzuia kutetea taji hilo ndio maana nimeanza kufanya maandalizi ya msimu ujao,”alisema Gomes.

Kocha huyo alisema hivi sasa yupo katika mazungumzo muhimu na uongozi wake kuhusu kukiboresha kikosi chao na aina ya wachezaji ambao wamepanga kuwaongeza ambao uwezo wao utakuwa tofauti kutokana na malengo waliyokuwa nayo.

Alisema mafanikio waliyoyapa msimu huu yanahitaji juhudi kuyaendeleza msimu ujao na hiyo inahitaji umakini mkubwa, hasa katika kipengele cha usajili, ambacho ndio chenye kuonesha ubora wa timu na upatikanaji wa matokeo mazuri.

Gomes alisema kwa ushindani wa ndani hana shaka kwamba timu yake imetawala na haina mpinzani ndio maana yeye na uongozi wameweka nguvu zao zaidi kwenye michuano ya kimataifa, ambayo anaamini itazidi kuwapandisha na kujulikana Afrika.

Kocha huyo tayari ametoa mapendekezo ya kuongeza wachezaji wawili kutoka nje, mmoja beki wa kati na wa pili ni kiungo mshambuliaji wote kutoka nje, ambao watachukua nafasi ya Francis Kahata na mwingine ni Mzimbabwe Parfect Chikwende anayedaiwa atatolewa kwa mkopo ili nafasi yake aweze kusajili mchezaji mwingine wakigeni.

Habari

Biashara

Burudani

Afrika

Maoni