Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 17Article 558019

Habari za michezo of Friday, 17 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Gomez: Simba ipo tayari kwa mikiki

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes

WAKATI Simba ikitarajiwa kuwasili leo jijini Dar es Salaam ikitokea mkoani Arusha, kocha wa timu hiyo, Didier Gomez amesema kikosi chake kipo tayari kwa mikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Simba wanawasili leo saa saba mchana tayari kwa mchezo wao wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe kwenye maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Simba (Simba Day).

Gomez akizungumza na gazeti hili jana muda mfupi baada ya mazoezi ya asubuhi, alisema kambi yake ya mkoani Arusha imefanikiwa kwa asilimia kubwa na sasa wanakuja Dar es Salaam wakiwa sawa kwa asilimia kubwa.

"Michezo miwili ya kirafiki tuliyocheza huku imetuonyesha wapi tulipo kwa sasa, tunarejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wetu na TP Mazembe pamoja na maandalizi ya mwisho mwisho kuelekea kwenye Ligi Kuu, nashukuru tulichokuwa tunakitaka kwenye kambi tumefanikiwa kukipata," alisema Gomez.

Alisema mchezo dhidi ya Mazembe nao utakuwa kipimo kizuri na aliwapa hamasa mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ikiwa ni siku yao maalum.

Mazembe kutua kesho

Katika hatua nyingine,TP Mazembe wanatarajiwa kutua nchini kesho saa saba mchana wakiwa na kikosi kamili tayari kwa mchezo huo wa Simba Day.

Kaimu Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema timu hiyo imesogezewa mbele mchezo wao wa Ligi Kuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa wiki moja ili kutoa nafasi kwao ya kuumana na Simba kwenye tamasha la 'Simba Day'.

"Mazembe tayari wametupa uthibitisho rasmi wa kutua kesho mchana, awali walikuwa na mchezo wa ligi siku hiyo ya Septemba 19, lakini kwa kutambua ukubwa wa Simba na ushirikiano mzuri uliopo baina ya timu hizi, waliomba kwa shirikisho lao la soka kusogezwa mbele na imekuwa hivyo," alisema Kamwaga.

Alisema kuwa makocha wa timu zote mbili watakutana na waandishi wa habari kesho saa tisa alasili kwa ajili ya kuzungumzia maandalizi yao kiufundi kuelekea kwenye mchezo huo.

Yazindua Mascot

wametambulisha Mascot rasmi wa klabu hiyo watakaojulikana kama Mo rafiki kwa lengo la kuongeza hamasa pindi timu iwapo uwanjani kwenye mechi mbalimbali kuanzia msimu 2021/22.

Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii klabu hiyo ya Simba wameandika kuwa: “Atakuwepo kwenye michezo yetu na kwa kuanzia utakutana nae siku ya Simba Day.”