Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 10 02Article 560857

Soccer News of Saturday, 2 October 2021

Chanzo: Mwanaspoti

Huyo Kanoute, apewe muda mtaona

Sadio Kanoute Sadio Kanoute

Kama unamchukulia poa kiungo chipukizi mpya wa Simba, Sadio Kanoute kutoka Mali, basi pole yako kwani mmoja wa mastaa aliocheza nao katika klabu ya Stade Malien aliyepo Namungo kwa sasa, Agiri Ngoda amesema jamaa akipewa muda Wanamsimbazi watapata raha kwani anajua sana soka.

Simba imemsajili Kanoute aliyerejea uwanjani baada ya kuumia na kutolewa kwenye pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, akitokea Al Ahli Benghazi ya Libya ikiwa ni miezi mitatu tu tangu aondoke Malien.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoda aliyezaliwa Machi 14, 2002, alisema Kanoute alikuwa miongoni mwa wachezaji hatari ambao aliwakuta Stade Malien alikocheza kwa kipindi kifupi kabla ya kwenda Tunisia kujiunga na CS Hammam-Lif.

“Japo sikukaa naye sana, lakini naweza kusema ni miongoni mwa wachezaji wakubwa niliowakuta klabuni hapo na jamaa ana uwezo wa kuituliza timu. Ni mzuri kwenye kunyang’anya mipira, nadhani atawasaidia sana Simba,” alisema nyota huyo wa timu ya taifa ya vijana.

“Jambo muhimu naloweza kusema ni Simba wampe muda kwani ligi yetu ni tofauti kabisa na Mali ambako nilimkuta huku miundombinu yetu bado, ni viwanja vichache sana ambavyo viwango vipo juu.”

“Uwezo wa kucheza hapa anao na hilo sina shaka nalo hata kidogo, japo mazingira ni tofauti ila mpira ni ule ule. Shikeni maneno yangu, anaweza kuwa mchezaji muhimu kwa Simba baada ya michezo michache ijayo,” alisisitiza mchezaji huyo aliyerejea nchini na kujiunga Namungo akitokea CS Hammam-Lif na kufafanua kilichomrudisha. “Korona kwa wenzetu imepamba moto sasa klabu nyingi zinaonekana kuathiriwa, sikuwa na chaguo lingine zaidi ya kuchukua uamuzi wa kurudi.”