Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 19Article 572746

Soccer News of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ilikuwa likizo ya moto kwa makocha hawa

Pablo alikua na kazi ya kukisoma kikosi chake Pablo alikua na kazi ya kukisoma kikosi chake

Baada ya mapumziko mafupi, uhondo wa Ligi Kuu unarejea upya, lakini unaambiwa huko nyuma ilikuwa ni likizo ya mtiti, moto na maumivu kwa baadhi ya makocha katika kusahihisha makosa kwa timu zao na kurejea kwa nguvu mpya.

Ligi Kuu ilikuwa imesimama kupisha kalenda ya shirikisho la soka duniani (Fifa) na sasa burudani inarejea kuanzia Ijumaa kwa baadhi ya mechi kurindima.

Hadi michuano hiyo inasimama, Yanga ndio walikuwa kileleni kwa pointi 15 baada ya kucheza mechi tano sawa na timu zote, lakini haikupoteza hata moja, huku ikifungwa bao moja na kufunga tisa.

Orodha ya baadhi ya timu na makocha wake ambao huenda likizo hiyo ilikuwa ‘mzigo’ kuhakikisha wanarekebisha udhaifu.

SIMBA

Licha ya kushika nafasi ya pili kwa pointi 11, lakini makocha wa timu hiyo huenda hawakuwa na raha kwa kipindi chote cha mapumziko mafupi wakihaha kurejesha furaha kwa mashabiki.

Simba ambayo inatetea ubingwa kwa msimu wa tano sasa, haijawa na ushawishi kwa mashabiki wake kama ilivyozoeleka misimu iliyopita na kuzua wasiwasi.

Hata hivyo, ushindi wake msimu huu umekuwa ni wa kusuasua, timu inapata matokeo kwa shida na kuwapa wakati mgumu makocha wake.

Awali, timu hiyo ilikuwa chini ya kocha Didier Gomes aliyefikia makubaliano na mabosi kusitisha mkataba na kumuachia kibarua, Hitimana Thiery, ambapo kwa sasa tayari ameshushwa Kocha Mkuu, Pablo Franco kutoka Hispania.

Pablo na wasaidizi wake huenda hawakuwa na furaha wakipambana kusuka upya kikosi ili kurejea makali yao.

TANZANIA PRISONS

Moja ya timu ambazo msimu huu mambo yamekuwa mazito ni pamoja na Wajelajela, ambao kiuhalisia hali si shwari na ni dhahiri hawajawa na furaha kwa kipindi chote cha mapumziko.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga lazima kwa muda wote amekuwa ‘bize’ kutafuta mwarobaini wa namna timu yake itaweza kujinasua mkiani na kufufua matumaini.

Prisons ndio wanaburuza mkia kwa pointi mbili baada ya mechi tano, hali ambayo inawapa hofu mabosi, wadau na mashabiki wake wakidhani chama lao linaenda kupotea.

Matokeo hayo yanamweka kwenye presha Mayanga kupambana kuhakikisha wanaporejea uwanjani kesho dhidi ya ndugu zao Mbeya Kwanza wanaleta mabadiliko, vinginevyo mambo yanaweza kuwa mazito zaidi.

AZAMA FC

Bado Azam haijaonyesha uhalisia wake msimu huu na hali hii inamuweka pabaya kocha wake, George Lwandamina katika kuweka mambo sawa.

Azam ambayo kwa sasa ipo nafasi ya nane kwa pointi saba, haina matokeo mazuri kulinganisha na mazingira ya klabu kwa ujumla hivyo lazima likizo hii haikuwa ya furaha kwake.

Timu hiyo iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, msimu huu matokeo yake hayajawa mazuri na inaporejea ligi mashabiki wa timu hiyo wanatarajia mabadiliko.

Lwandamina anapaswa kudhihirisha ubora wa klabu unaoendana na uhalisia wa matokeo uwanjani, vinginevyo anaweza kujikuta nje kama waajiri wake watashindwa kuvumilia.

KMC

Timu hii msimu huu mambo yamewawia magumu sana kwani katika mechi tano walizocheza, wameambulia alama mbili tu na kukaa nafasi mbili za mkiani, huku ikiwa kati ya timu zilizoruhusu mabao mengi (6).

KMC ambayo iliwahi kutesa na kumaliza nafasi nne za juu na kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, msimu huu mambo yamekuwa ndivyo sivyo na kuzua wasiwasi wa kushuka daraja.

Ni wazi kuwa kocha mkuu wake, Habibu Kondo atakuwa na kazi ngumu kuhakikisha wanaporejea uwanjani wanakuja kivingine na kurejesha heshima ya klabu.

MTIBWA SUGAR

Hawajawa na matokeo mazuri na hii imeongeza zaidi presha kuanzia kwa mashabiki hadi mabosi wa timu hiyo kutokana na nafasi waliyopo kwenye msimamo.

Mtibwa, timu kubwa na kongwe hapa nchini msimu huu haijaonyesha makeke yoyote na wengi wameanza kuitabiria mapema kushuka daraja kutokana na kile walichonacho kwa sasa.

Licha ya kuanza bila kocha mkuu, lakini miamba hiyo ya mji kasoro bahari, Morogoro inayo kazi nzito haswa kocha wake, Joseph Omog atakuwa anakuna kichwa kujua namna ya kurejea uwanjani, kocha anatakiwa kurejesha matumaini kwa mashabiki wao kwa kufanya tofauti.

GEITA GOLD

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu, timu hii ya mkoani Geita bado haijashawishi haswa kwa upande wa matokeo waliyonayo kuwashangaza wengi wanaohoji hatma yao msimu ujao.

Tayari mabosi wa timu hiyo walishafanya uamuzi mzito walipomtimua aliyekuwa kocha wake, Ettiene Ndayoragije hivyo msala wote kwa sasa upo kwa mzawa, Fredy Felix Minziro.

Geita Gold katika mechi tano ilizocheza imekusanya pointi mbili na kukaa nafasi ya 13, hivyo Minziro atakuwa ametumia muda wa mapumziko mafupi kuamsha mzuka nyota wake kuhakikisha wanarejea salama.

NAMUNGO

Vijana hawa wa Ukanda wa Kusini lazima kipindi cha mapumziko hawakula bata wala kufurahia kitu, kwani matokeo waliyoyapata si rafiki sana kwao kuinjoi.

Pointi tano katika michezo mitano sawa na wastani wa alama moja kila mechi haiwezi kumfanya kocha wake, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuwapa likizo nyota wake kula bata mjini.

Namungo ambayo msimu uliopita iliwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho, bado hawajaonyesha ubora wao katika mechi tano, hivyo likizo hii watakuwa wamepata msoto.

COASTAL UNION

Walionyesha mchezo wa kiushindani haswa walipokutana na Simba na kulazimishana nao sare ya bila kufungana, lakini hali yao si shwari.

Kocha Mmarekani Mellis Medo huenda atakuwa amekaa na nyota wake na kuweka mikakati namna ya kurudi uwanjani baada ya likizo hii kumalizika.

Medo ambaye msimu uliopita alishuka daraja na Gwambina, lazima atakuwa ametumia vyema likizo hii kurekebisha kasoro zilizoonekana kwa wachezaji wake ili kuiinua timu yake.

MAKOCHA WAFUNGUKA

Kocha Mkuu wa KMC, Habibu Kondo anasema licha ya kuanza kwa kusuasua haswa kuapata matokeo yasiyoridhisha, lakini anaamini wanapoianza tena ligi wanaenda kuleta mabadiliko.

“Ni kweli tumeanza vibaya msimu lakini kwa mapumziko haya kuna kitu tumekifanya haswa kusahihisha pale ilipoonekana upungufu, tunajiandaa na mechi ya raundi ya sita dhidi ya Azam,” anasema Kondo.

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga anasema kuwa; “Timu haina upungufu mkubwa isipokuwa ni upepo tu kukosa matokeo mazuri tunayoyataka, ila naamini kwa maandalizi tuliyoyafanya kwa muda huu wa likizo fupi tutafanya vizuri na kukaa nafasi nzuri.”