Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 30Article 560611

Soccer News of Thursday, 30 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Je ushabiki husababisha vifo vya ghafla?

Je ushabiki husababisha vifo vya ghafla? Je ushabiki husababisha vifo vya ghafla?

WIKI hii hapa nchini gumzo kubwa lililotawala ni mechi ya watani wa jadi ya kuwania ngao ya jamii kati ya Simba na Yanga ambapo timu ya Wananchi wa Jangwani ilitwaa tuzo hiyo kwa kumchapa Mnyama bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Mkapa ni kawaida kubeba hisia za maelfu ya mashabiki ndani na nje ya nchi ikiwamo wanaotazama mechi moja kwa moja au wanaofuatilia kwa njia ya redio na runinga.

Burudani ya soka hubeba hisia za juu za mashabiki kiasi kwamba huwa ni kawaida wengine kuumia kihisia au kujikuta wakipoteza fahamu kutokana na mshtuko wa furaha au karaha. Tukio la kusikitisha ni lile wilayani Mpwapwa la kufariki dunia ghafla kwa polisi aitwaye Rashidi Mohammed Juma wakati anatazama mechi kwenye runinga.

Shabiki huyo alianza kujisikia vibaya ghafla na alionekana kujishika eneo la kifuani ambapo sekunde chache baadaye alianguka huku akikoroma na kupoteza fahamu.

Baadaye alichukuliwa na kupelekwa katika huduma ya afya alikobainika kuwa tayari alikuwa ameshafariki dunia. Kwa mujibu wa shuhuda aliyekuwa naye wakati wakitazama mechi hiyo alieleza kuwa alianza kujisikia vibaya muda mfupi kabla ya Yanga kupata bao hilo.

Kifo hicho kimeleta maswali mengi mitandaoni na mitaani ambako watu wengi hawafahamu masuala ya afya kwa undani. Huwa ni kawaida kwa jamii kujiuliza pale yanapotokea matukio kama haya na wengi hupata hofu.

Je ni kweli hisia kali za ushabiki zinaweza kusababisha kifo cha ghafla? Jibu inawezekana, lakini sio moja kwa moja ila tu hisia huweza kusababisha mshtuko wa moyo. Kwa kawaida binadamu anapopenda jambo fulani na kumganda moyoni ikiwamo kumkaa akili mwake ni suala la kawaida. Hali kama hii inaweza kumletea kuumia kihisia ikiwamo hisia chanya au hasi.

Binadamu anapotazama kitu anachokipenda macho huona, kisha picha hiyo huenda kutafsiriwa katika ubongo na hatimaye hujibu mapigo ikiwamo kufurahi au kukasika sana.

Mambo haya yanaweza kusababisha mwili kitiririsha vichochezi ambavyo huusababishia mwili kupata mshtuko unaoweza kusababisha moyo kusimama. Pale hatua za huduma ya kwanza zinapochelewa kumfikia mtu, basi kifo kinaweza kutokea.

Leo nitatolea ufafanuzi tatizo la vifo vya ghafla ambalo shambulizi la moyo ni moja ya sababu zinazochangia watu kupata tatizo hili.

KINACHOSABABISHA VIFO GHAFLA

Shambulizi la moyo kitabibu kama ‘heart attack’ ni moja ya matatizo ya kiafya yasiyoambukiza yanayosababisha mara kwa mara vifo vya ghafla kwa watu wazima wa umri wa miaka 45 na kuendelea. Ni kawaida ikatokea sababu ya kifo cha ghafla isijulikane moja kwa moja, lakini yapo matatizo ya kiafya yanayohusishwa ikiwamo vinavyotokea usingizini.

Ukiacha matatizo ya moyo kwa ujumla. Katika sehemu nyingine za mwili yaani ubongo na figo vinaweza kupata matatizo ya kiafya na kusababisha kifo cha ghafla. Moyo ndiyo ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, magonjwa au matatizo yake huwa ni ya kimyakimya na yanaongoza kusababisha vifo vya ghafla duniani. Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimyakimya pasipo kujijua kwa anayeugua. Mara nyingi watu hugundulika kuwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.

Mara nyingi kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo ni sababu kubwa inayochangia matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo. Mishipa ya damu ya moyo ya ateri ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu au kupata kiasi kidogo. Uharibifu hutokana na mgando wa tando ya mafuta katika kuta za mishipa hii.

Hali hii husabisha misuli kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kwa ufanisi, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama. Misuli ya moyo kututumka pia ni sababu mojawapo kwani husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo ya kupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu. Sababu nyingine ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo ya kawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valvu za moyo na kuzaliwa na moyo wenye hitilafu.

Vilevile uwepo wa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kuwa na hitilafu ya mapigo ya moyo. Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo ni kama vile sumu, mrundikano wa taka sumu, matatizo ya mfumo wa hewa, ukwame wa kitu njia ya hewa, kuvuta hewa chafu na ajali katika ogani nyeti.

Watu walio katika hatari ya kupata tatizo hili ni pamoja na shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha lehemu, unene, kisukari, uvutaji tumbaku na kutofanya mazoezi, umri mkubwa (miaka 45+) na historia ya familia ya tatizo hili. Inawezekana mtu akawa na matatizo ya afya ya moyo, lakini asijijue, ila inapotokea mshtuko wowote ule ndipo unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi.

Usipuze unapoona dalili hizi ikiwamo maumivu ya ghafla ya kifua, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kuchoka kirahisi, uchovu, pumzi kukatika, kuona giza, kuishiwa nguvu, kupoteza fahamu, kichefuchefu, kutokwa jasho na kukosa usingizi.

Ni vizuri kuwa na utamaduni wa kuchunguza afya ya mwili mzima angalau mara moja kwa mwaka.