Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 25Article 559639

Soccer News of Saturday, 25 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kali 10 za watani

Kali 10 za watani Kali 10 za watani

HABARI ya mjini kwa sasa ni mechi ya Simba na Yanga inayochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni ya Ngao ya Jamii.

Kama ilivyozoeleka, mechi hiyo huwa na mvuto na ushindani wa aina yake na hiyo ni kutokana na historia ya timu hizo mbili pamoja na idadi kubwa ya mashabiki zilionao.

Hata hivyo, zipo mechi kati ya Simba na Yanga ambazo zilionekana kuwa na mvuto mkubwa zaidi na Mwanaspoti inakuletea orodha ya mechi 10 ambazo zilibamba zaidi hapo nyuma.

1. Simba 4-4 Yanga

- Novemba 9, 1996

Mechi hii ilikuwa na mvuto wa kipekee kutokana na idadi kubwa ya mabao yaliyofungwa ambayo yalikuwa nane (8) na kuwa mchezo wa watani wa jadi uliozalisha mabao mengi zaidi katika historia.

Simba siku hiyo walikomboa bao ‘usiku’ kupitia kwa Dua Said aliyefunga katika dakika ya 90 na mechi kumalizika kwa sare ya 4-4 kwenye Uwanja wa Sheikh Amr Abeid, Arusha.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Thomas Kipese, Ahmed Mwinyimkuu na Dua Said ambaye siku hiyo alitupia mara mbili likiwamo la dakika ya mwisho ya mchezo lililowaokoa Simba na kichapo.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Edibily Lunyamila (penalti), Said Mwamba ‘Kizota’ na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’, huku Mustapha Hoza wa Simba akijifunga.

2. Yanga 3-3 Simba

- Oktoba 20, 2013

Ni mechi ambayo iliweka rekodi ya kila timu kufunga mabao matatu katika kila kipindi na kuifanya imalizike kwa sare ya mabao 3-3

Yanga ilitangulia kupata mabao yake kupitia kwa Mganda Hamis Kiiza aliyepachika mawili huku Mrisho Ngassa akitupia jingine.

Hata hivyo, katika kipindi cha pili kilikuwa cha Simba ambayo ilisawazisha mabao yote matatu kupitia kwa Joseph Owino, Bertram Mwombeki na Gilbert Kaze.

3. Simba 1-1 Yanga

- Machi 5, 2011

Katika mechi hii, mwamuzi Oden Mbaga alilazimika kutumia luninga kubwa ya uwanjani kuruhusu bao la kusawazisha la Simba lililofungwa na Musa Mgosi katika dakika ya 74 baada ya awali kulikataa akidai mfungaji aliotea.

Awali, Yanga ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Stephano Mwasyika kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 56.

4. Simba 1-2 Yanga

- Agosti 10, 1974

Mechi hii ilichezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Sunday Manara na Gibson Sembuli wakati lile la Simba lilipachikwa na Adam Sabu.

Katika mechi hiyo, historia inasema kuwa shabiki mmoja wa Simba alijitupa kwenye pipa la mafuta na kufariki baada ya timu yake kufungwa.

Lakini pia mchezaji Saad Ally wa Simba alianguka uwanjani na kuzirai, kiasi cha kuwahishwa hospitali ya Bugando. Hapo ndipo hadithi zinadai kuwa alipoangukia hapakuota tena nyasi hadi leo, ambapo kumewekwa nyasi bandia.

5. Yanga 2-0 Simba

- Agosti 5, 2000

Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga. Mechi imeingia kwenye zile ya kukumbukwa zaidi kwa sababu moja tu. Mfungaji wa magoli yote mawili alikuwa ni Idd Moshi. Alifunga magoli hayo akiwa anatoka kwenye fungate ya ndoa yake.

6. Simba 2-1 Yanga

- Julai 23, 1988

Yanga ilihitaji japo sare ili kutwaa ubingwa wakati Simba haikuhitaji kitu kingine zaidi ya ushindi ili kuepuka kshuka daraja. Baada ya Edward Chumila kuifungia Simba na Issa Athumani kuisawazishia Yanga, John Makelele ‘Zig Zag’ dakika ya 58 aliifungia Simba bao muhimu lililowabakisha Wekundu wa Msimbazi kwenye ligi, Yanga ikikosa ubingwa uliokwenda kwa Coastal Union.

7. Yanga 1-0 Simba

Julai 10, 2011

Mchezo wa Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati wa Julai 10,2011 uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0, ndio ambao umeandika historia ya bao la dakika za mwisho zaidi timu hizo zilipokutana ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Bao hilo lilifungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Kenneth Asamoah katika dakika ya 109 akimalizia krosi ya Rashid Gumbo katika mchezo huo ulichezwa kwa dakika 120.

8. Yanga 1-2 Simba

- Februari 25, 2017

Ni moja ya mechi za kusisimua ambazo zilikutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga.

Licha ya Yanga kutangulia kupitia kwa Saimon Msuva kwa mkwaju wa penalti, Simba huku wakiwa pungufu, walisawazisha na kufunga bao la pili la ushindi.

9. Simba 1-1 Yanga

- Oktoba Mosi, 2016

Katika mchezo huo, Yanga ilitangulia kupata bao lililozua utata kupitia kwa Amissi Tambwe ambaye kabla hajafunga aliushika mpira kwa mkono na kuukwamisha wavuni

Hata hivyo, dakika zikiyoyoma, Shiza Kichuya aliyekuwa moto enzi hizo alipiga mpira wa kona ulioenda moja kwa moja wavuni na kuisawazishia Simba bao na matokeo kumalizika kwa sare huku Simba wakiwa pungufu baada ya nahodha wao Jonas Mkude kuonyeshwa kadi nyekundu na refa Martin Saanya.

10. Simba 2-2 Yanga

- Septemba 28, 2003

Baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ulifanyika miezi minne nyuma yake, wengi walitamani kuona kama Simba ingelipa kisasi.

Simba waliingia kwa kasi na kupata mabao mawili ya mapema yaliyofungwa na Emmanuel Gabriel (dk 27 na 36) na kumfanya kila mmoja aamini kwamba wangeibuka na ushindi mnono na kulipa kisasi kwa Yanga.

Hata hivyo, baadaye mambo yaligeuka, Yanga walipata bao la kwanza kupitia kwa Kudra Omary (dk.42) na dakika ya 55 walisawazisha kupitia kwa Heri Morris.