Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 16Article 551788

Soccer News of Monday, 16 August 2021

Chanzo: eatv.tv

Kamwaga awajibu wakosoaji, usajili Simba

Clatous Chama anatajwa kujiunga na RS Berkane ya Morocco Clatous Chama anatajwa kujiunga na RS Berkane ya Morocco

Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Wa Klabu ya Simba Ezekiel Kamwaga ametoa ufafanuzi juu ya taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ya kuwaaga wachezaji Clatous Chama na Luís Miquissone ambao wameondoka klabu hapo, hii ni mara baada ya taarifa hiyo kukutana na ukosoaji.

Taarifa iliyotolewa na Simba leo asubuhi ikielezea taarifa za wachezaji hao kuondoka ilikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wadau wakihoji kwa nini taarifa hiyo haijataja wachezaji hao wanaenda wapi wala haijataja dau lilitumika kuwanunua.

Sasa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram Kamwaga ameandika;

''Kuna watu wanahoji kwa nini taarifa ya Simba SC haijasema gharama za mauzo au timu wanazokwenda Chama na Miquissone. Si lazima klabu kutaja gharama ilizotumia kuuza au kununua mchezaji. Hata katika ligi zilizoendelea duniani, bei huwa hazitajwi kwa kila mauzo. Kwenye Kiingereza huwa wanasema Undisclosed. Wakati Marouane Fellaini anatoka Everton kwenda Manchester United, bei haikutajwa. Iko hivi, kuna sababu za kusababisha gharama kutajwa na kuna sababu za kusababisha gharama zisitajwe. Ni kawaida kabisa kwenye mpira.

Kwa upande mwingine akatoa ufafanuzi juu ya kwanini taarifa hiyo haijasema wanakwenda kujiunga na vilabu gani;

''Si lazima pia. Kila timu ina utaratibu wake wa kutangaza wachezaji wapya. Wanataka wawe wa kwanza kutangaza mchezaji mpya na wanafaidika na hilo. Wanachotaka wewe wauzie mchezaji na wao watatangaza wenyewe. Mnakubaliana hivyo. Sasa, katika mazingira hayo, Simba SC haiwezi kusema wanaenda wapi kwa sababu itakiuka makubaliano. Muda si mrefu itajulikana wanaenda wapi. Na ungekuwa mkanganyiko zaidi kwenye taarifa moja tungesema huyu anaenda kule na huyu hatusemi. Taarifa imeondoa huo mkanganyiko.''

Akamaliza kwa kuandika ''Bado tuna safari ndefu kwenye kujifunza haya masuala ya transfers. Tuendelee kujifunza.''

Licha ya taarifa hiyo ya Simba kutoweka wazi wachezaji hao wanaelekea wapi lakini kwa mujibu wa taarifa za usajili Luiz Miquisson anatajwa kujiunga na Al Ahly ya Misri na Chama ameonekana akiwa na jezi ya RS Berkane ya Morocco.