Uko hapa: NyumbaniMichezo2019 11 15Article 488032

Sports News of Friday, 15 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Kete ushindi Taifa Stars mikononi mwa Samatta, Msuva

Kete ushindi Taifa Stars mikononi mwa Samatta, Msuva

Dar es Salaam. Ubora wa washambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta na Saimon Msuva umebeba matumaini ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ dhidi ya Guinea ya Ikweta leo, saa 1:00 usiku, katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021.

Taifa Stars ipo Kundi J pamoja na Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta katika kampeni ya kuwania kufuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Cameroon.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije anaingia katika mchezo huo huku silaha zake za mafanikio akiwa nahodha Samatta na Msuva.

Wachezaji hao wamefunga mabao 10 kati ya 13 yaliyofungwa na Stars tangu mwaka jana, ambapo kila mmoja amepachika mabao matano na kwa kiasi kikubwa yaliisaidia Stars kufuzu fainali za Afcon mwaka huu zilizofanyika Misri pamoja na na tiketi ya kucheza hatua ya makundi kusaka kucheza Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022.

Wakicheza katika kiwango cha juu wiki tatu zilizopita huku wakifunga mabao katika klabu zao, jambo hilo linatoa matumaini kuwa huenda wakahamishia kasi hiyo katika mchezo dhidi ya Guinea ya Ikweta.

Akizungumzia maelewano yake na Samatta, Msuva alisema yametokana na kuendana kiuchezaji.

“Huwa sipati shida kabisa kucheza naye mbele kwa sababu najua namna gani ya kucheza, kuna muda huamua kuniacha nisimame mbele peke yangu, Sam ni mjanja hutaka kuwadanganya kidogo mabeki,” alisema Msuva.

Naye Samatta alisema: “Nafurahia kucheza naye (Msuva), napenda kasi yake katika kushambulia. Naamini Mungu atamfungulia njia na yeye apate nafasi ya kucheza Ulaya.”

Akiuzungumzia ushirikiano wa wawili hao katika safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars, Kocha Abdallah Kibadeni alisema unatoa jibu kuwa kuna umuhimu wa wachezaji wa Tanzania kupata nafasi kwa wingi katika ligi zenye ushindani zaidi.

“Samatta anacheza Ulaya, amejengeka sana kiushindani, pamoja na kuwa Msuva hachezi Ulaya bado Ligi ya Morocco ni kubwa, kwa ushirikiano na wachezaji wengine tunaweza kufanya vizuri, kikubwa ni kocha kuwa na mbinu bora hasa tukizingatia tupo nyumbani,” alisema nyota huyo wa zamani wa Simba.

Mbali ya Samatta na Msuva, pia Kocha Ndayiragije atakuwa na mshambuliaji Eliuter Mpepo wa Buildcon ya Zambia ambaye amekuwa na kiwango kizuri tangu ajiunge na timu hiyo.

Tumaini jingine ni kasi na nguvu aliyoonyesha mshambuliaji Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania katika mchezo kati ya Stars na Sudan hivi karibuni, na iwapo kocha atatumia washambuliaji watatu huenda akawa msaada mkubwa kikosini.

Pamoja na hayo bahati nzuri kwa Samatta, Msuva na washambuliaji wengine wa Stars ni kwamba, Guinea ya Ikweta imekuwa na safu ya ulinzi ambayo hushindwa kuhimili presha ya mashambulizi hasa inapokutana na washambuliaji wenye kasi, jambo linaloweza kuwa faida kwa Tanzania. Wakati Samatta na Msuva wakibeba matumaini ya Watanzania, wapinzani wao wanawategemea viungo Pedro Obiang wa timu ya Sassuolo ya Italia na Pablo Ganet wa Algeciras CF inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Hispania.

Washambuliaji wao tegemeo ni Emilio Nsue wa Apollon ya Cyprus mwenye uwezo pia wa kucheza kama beki na kinda Secundino Eyama Nsi anayecheza klabu ya Manzanares CF inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu, Hispania. Nyota wao anayepaswa kuchungwa zaidi ni Nsue ambaye ameshazichezea Middlesbrough na Birmingham City (England) na Mallorca (Hispania).

Join our Newsletter