Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 16Article 542896

Habari za michezo of Wednesday, 16 June 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kibu: Nikikata ya Yanga, inaingia ya Simba

Kibu: Nikikata ya Yanga, inaingia ya Simba Kibu: Nikikata ya Yanga, inaingia ya Simba

BAADA ya juzi kukiwasha kwa mara ya kwanza akiwa na Taifa Stars dhidi ya Malawi, nyota wa Mbeya City, Kibu Denis amewaingiza vitani mabosi wa Simba na Yanga ambao wameonesha nia ya kutaka saini yake.

Kibu ilimchukuwa dakika 31, tu kuonesha ubora wake na kuwavutia wapenzi wengi wa soka baada ya kuingia dakika ya 59 ya mchezo huo kuchukua nafasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyepumzishwa.

Baada ya kuingia, Stars ilirudisha uhai eneo la ushambuliaji akionekana kutulia akisaidiana na John Bocco na dakika ya 67 alitengeneza bao kwa kuchukua mpira, kuwatoka mabeki wa Malawi na kupiga pasi mpenyezo kwa Bocco aliyepasia nyavu na kuiandikia Stars bao la kuongoza.

Kibu hakupoa baada ya bao hilo kwani aliendelea kuwapa wakati mgumu mabeki wa Malawi kwenye kumkaba na dakika ya 73 akiwa katika harakati za kutengeneza bao la pili alipigwa buti nje kidogo ya eneo la boksi la 18 la Malawi na refa kuamuru ipigwe faulo iliyopigwa kiufundi na Israel Mwenda na mpira kuzama moja kwa moja nyavuni na Stars kumaliza mechi kwa bao 2-0.

Baada ya mechi hiyo kumalizika, kila shabiki aliyekuwa uwanjani alikuwa akiliimba jina la Kibu.

Kibu amelidokeza Mwanaspoti kuwa usiku wa kuamkia jana hakulala kutokana na simu yake kuita muda wote na kila akipokea alikutana na watu waliojitambulisha kuwa wametoka Simba na Yanga.

“Nimepokea simu kutoka pande zote mbili lakini hakuna tulichozungumza zaidi ya kuwataka wafuate taratibu, nadhani hiyo njia sahihi zaidi ya kunipigia simu mara kwa mara,” alisema Kibu na kuongeza:

“Sipendi sana kuzungumzia mambo haya lakini timu yeyote ile naweza kuichezea kikubwa kuwe kuna haki na taratibu zote zimezingatiwa,” alisema.

Hadi sasa Kibu, ndiye anaongoza kwa upachikaji mabao Mbeya City msimu huu akiwa amefunga bao sita licha ya kutocheza kama nusu ya mechi za timu hiyo.

Alijiunga Mbeya City msimu huu akitokea Geita Gold iliyopanda Ligi Kuu msimu huu ambayo ilimsajili kutoka Kumuyange FC ya Ngara iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) miaka mitatu iliyopita.