Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 07 16Article 547180

Habari za michezo of Friday, 16 July 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kisa watani... Nyasi zawekewa ulinzi Kigoma

Kisa watani... Nyasi zawekewa ulinzi Kigoma Kisa watani... Nyasi zawekewa ulinzi Kigoma

KUELEKEA pambano la Simba na Yanga, Julai 25, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, ulinzi mkali umewekwa uwanjani hapo kuzuia watu wanaokwenda kufanya mambo ya kishirikina.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa Kigoma (KRFA), Omari Gindi amesema kuwa kumekuwa na kupishana kwa watu wanaofika uwanjani hapo wakichukua mchanga na nyasi katika sehemu mbalimbali za uwanja ikiwemo ndani ya eneo la kuchezea na kuchukua nyasi.

Akizungumza mjini hapa uwanjani hapo, Gindi alisema kuwa kutokana na hali hiyo kwa sasa wamezuia watu wasiohitajika kuingia uwanjani hapo bila sababu maalumu na kuanzia jana nyasi zitakuwa na walinzi maalumu na hakuna mtu kuingia wala kuzigusa mpaka siku ya mchezo.

“Naamini mazoezi ya walimu na hali ya wachezaji ndio yanayoweza kuleta matokeo. Kwa sisi kama chama cha soka hatuamini kwenye mambo ya ushirikina na hivyo tumezuia wote ambao wanataka kuingia uwanjani kwa ajili ya jambo hilo,” alisema Gindi na kusisitiza kwamba hawatapendelea upande wowote isipokuwa wanachotaka ni mechi ichezwe ndani ya dakika 90.

Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi ni mashabiki au watu wa klabu gani kati ya Simba na Yanga waliokwenda kufanya imani hizo za kishirikina, lakini alikemea hali hiyo na kuomba watu wasijihusishe na masuala hayo kwani hayana afya kwenye soka.

Akizungumzia maandalizi na marekebisho yanayofanyika uwanjani hapo, alisema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na kwa sasa wanamalizia kujenga jukwaa la mashabiki wakaosimama na ukarabati wa vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kuweka sawa eneo la kuchezea ambalo limekidhi vigezo kwa taratibu za Shjirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Alisema uwanja huo unatarajia kuingiza mashabiki 17,000 watakaokaa na watakaosimama.

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) yanaendelea vizuri na kwa sasa uthibitisho ni kwamba mechi hiyo itachezewa Lake Tanganyika.

Madadi alisema ukaguzi umefanyika na marekebisho madogo yanafanywa, lakini amebainisha kuwa kazi kubwa imefanya na serikali kwa kushirikiana na wamiliki wa uwanja, CCM Mkoa Kigoma na KRFA ili kuhakikishaa kwamba taratibu zote za mchezo zinafanyika uwanjani hapo.

“Kwa kifupi imekubalika fainali itafanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani hapa na Ijumaa kutakuwa na kikao baina ya serikali ya mkoa,” alisema Madadi ambaye kitaaluma ni kocha wa soka.

Mechi hiyo ya watani wa jadi, Simba na Yanga imekuwa na hamasa kubwa kwa mashabiki mkoani hapa huku kila upande ukitamba kubeba ndoo. Ushabiki mkubwa kwenye mechi hiyo unachagizwa na Yanga kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu bara baina ya timu hizo hivi karibuni.