Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 30Article 554395

Soccer News of Monday, 30 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kocha Simba Queens awahofia Waganda

Kocha Simba Queens awahofia Waganda Kocha Simba Queens awahofia Waganda

KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Hababuu Ali amesema licha ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya PVP FC ya Burundi katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Cecafa kwa wanawake uliochezwa katika Uwanja wa Nyayo, Kenya hawezi kubweteka kwani anakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Lady Doves kutoka Uganda.

Simba sasa inahitaji pointi tatu kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inafanyika Nairobi, Kenya.

Akizungumza kwa njia ya mtandao jana, Hababuu alisema mchezo dhidi ya Lady Doves utakaochezwa kesho ni kama fainali kutokana na aina ya timu wanayokwenda kukutana nayo, lakini pia kama watashinda mchezo huo watakata tiketi ya kuingia katika hatua ya nusu fainali.

“Nashukuru Mungu wachezaji wangu wamefanya kile tulichofanyia kazi kwenye mazoezi, lakini hatupaswi kufanya makosa ili kutimiza malengo yetu ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.”

“Ndio maana nililazimika kumtoa mlinda mlango namba moja baada ya kushindwa kuvumilia makosa aliyokuwa akifanya ambayo hayapaswi kufanyika katika michuano mikubwa kama hii,” alisema Hababuu.

Lady Doves inaongoza Kundi A ikiwa na pointi tatu sawa na Simba Queens, lakini wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga kwani waliifunga FAD kwa mabao 5-0, wakati Simba walishinda 4-1.

PVP wao watacheza dhidi ya FAD na mechi zote zitachezwa Uwanja wa Kasarani.

Wawakilishi wa Zanzibar, New Generation walifungwa na Yei Joint Stars ya Sudan Kusini kwa mabao 2-1.