Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 30Article 554446

Soccer News of Monday, 30 August 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

"Kuna faida zaidi kwenye kupoteza Mchezo wa kirafiki kuliko kushinda" Oscar Oscar

Oscar Oscar, Mchambuzi wa Masuala ya Soka Oscar Oscar, Mchambuzi wa Masuala ya Soka

Klabu ya Yanga imecheza mechi yao ya kirafiki kwa mara ya kwanza tangu wafanye usajili wa nyota kadhaa katika kikosi chao ikiwa ni maandalizi ya msimu ujao katika michuano ya ligi kuu Tanzania bara na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mechi yao ya kwanza wamecheza na klabu ya Zanaco kutoka nchini Zambia katika maadhimisho ya kilele cha "Wiki ya Mwananchi" yaliyofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga imepoteza kwa magoli 2-1 ambapo katika mchezo huo ilitumia baadhi ya nyota wake kadhaa waliosajiliwa katika dirisha hili kubwa la usajili linaloendelea.

Kutokana na kipigo hicho kuna maoni tofauti kutoka kwa Wapenzi, Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo.

Wapo ambao wamechukulia kipigo hicho kwao sio kitu kwa kuwa ndio kwanza wanajenga timu ukizingatia hawakuwahi kucheza mechi yoyote kujipima ubora na muunganiko wa kikosi chao kabla ya mechi hiyo.

Kuna wale waliosikitishwa na kipigo hicho na kuona msimu huu pia wanaweza wasifue dafu mbele ya watani zao Simba ambao wamebeba ubingwa kwa misimu minne mfululizo.

Sasa Mwanahabari wa habari za michezo na Mchambuzi wa masuala ya soka nchini Oscar Oscar Jr, ametoa mtazamo wake kwa namna Yanga ilivyocheza katika mechi hiyo.

"Mimi sijatazama kama ni mechi ambayo Yanga walikua wanaihitaji sana kupata matokeo, kwa nilichokiona jana Yanga wana wachezaji lakini hawana timu, na ili kupata timu mwalimu inapaswa afanye kazi ya ziada"

"Kwa kile kilichotokea jana ni faida kwa Yanga kuliko hasara, pengine ushindi ungewaaminisha uongo na kuona tayari wamemaliza kumbe wana mlima mrefu, wachezaji wanaonekana bado miili yao haijafunguka kwa sasa na kadri wanavyokwenda mbele watakua vyema" amesema Oscar

Nyota kadhaa wa Yanga walipata nafasi ya kuonesha makali yao uwanjani na kwa hesabu za haraka haraka wanaonekana wana uwezo wa kuleta mabadiliko katika kikosi cha sasa cha Yanga.