Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 29Article 554245

Soccer News of Sunday, 29 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Lwandamina awasifu mastaa Azam

Kocha Mkuu wa Azam George Lwandamina (kushoto) akitoa maelekezo Kocha Mkuu wa Azam George Lwandamina (kushoto) akitoa maelekezo

Kikosi cha Azam kipo nchini Zambia katika mji wa Ndola kilikoweka kambi kikijifua kwaajili ya msimu ujao ikiwa pamoja na kucheza mechi za kirafiki kupima timu yao.

Ikiwa huko, tayari ilishacheza mchezo mmoja dhidi ya Red Arrows na kuchapwa bao 4-0 lakini kocha mkuu wa timu hiyo, mzimbabwe George Lwandamina ameeleza kuwa kichapo kile hakimtishi bali kimempa funzo kuelekea msimu ujao.

Lwandamina ameeleza kuwa mechi ile alikuwa kwenye majaribio ya kutesti wachezaji wake wapya na tayari amepata dawa ya namna gani awatumie huku akitamba uwezo wao kuwa mkubwa zaidi.

“Mechi ile ilikuwa ya mwanzo kuangalia wapi maandalizi yetu yamefikia, tulitumia wachezaji tofauti na kugundua wapi tunakosea na tunahitaji kuongeaza kitu.

“Tatizo kubwa lililotokea katika mchezo ule ni wachezaji kuwa wazito kutokana na kufanya mazoezi mengi magumu kipindi tupo Tanzania hali ambayo kwa sasa imekuwa kawaida kutokana na mazoezi tunayoendelea kuyafanya,” amesema Lwandamina.

Sambamba na hilo, Lwandamina alijivunia vipaji vya wachezaji wapya katika kikosi hicho huku akijivunia uwepo wa washambuliaji wake wawili Prince Dube na Idris Mbombo.

“Hadi sasa wachezaji wapya wamezoeana na wenzao na wanaonyesha viwango bora mazoezini. Kila mmoja anajitoa kwa uwezo wake jambo ambalo linanipa imani kuwa msimu ujao tutakuwa na kikosi bora zaidi ya msimu uliopita,” amesema na kuongeza;

“Msimu uliopita tulikuwa tukipata tabu kwenye eneo la ushambuliaji zaidi pale Dube alipokuwa majeruhi, lakini sasa tumempata Mbombo ambaye ni bora kwenye kufunga pia hivyo nitakuwa na machaguo tofauti.

“Naweza kuwaanzisha wote kwa pamoja ama kumuanzisha mmoja na mwingine kupumzika hivyo nadhani tutakuwa na msimu bora zaidi,” amesema.

Kuelekea msimu ujao Azam imefanya usajili wa wachezaji wapya saba, watano wa kigeni ambao ni Paul Katema, Idris Mbombo, Keneth Muguna, Charles Zulu na Rogers Kola huku wazawa wakiwa wawili kipa, Ahmed Ali ‘Salulu’ na Edward Manyama.

Azam itaendelea kuwa Ndola hadi Septemba 5, na itacheza mechi kadhaa za kirafiki mpaka itakaporejea nchini Tanzania.