Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 24Article 544090

Habari za michezo of Thursday, 24 June 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Maafande kutibuliana mipango leo

Ruvu Shooting Ruvu Shooting

MAAFANDE wa Ruvu Shooting na wale wa Polisi Tanzania leo Juni 24 saa 10:00 jioni watakuwa wakipambana kutafuta alama tatu muhimu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara duru ya 31.

Mechi hii inatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na kila timu kutaka ushindi utakaoisogeza kwenye malengo yake wakati atakayepoteza mchezo huo atakuwa ametibuliwa mipango yake kuelekea ukingoni mwa ligi.

Wenyeji Ruvu wapo nafasi ya 12 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 31 na kuvuna alama 37, hivyo watahitaji ushindi ili kuendelea kukwepa panga la kushuka daraja kwani alama hizo zinaweza kufikiwa na timu tano zilizo chini yake kasoro Mwadui tu.

Polisi Tanzania wao wapo nafasi ya tisa wakiwa na alama 41 walizovuna kwenye mechi 31, hivyo leo wanahitaji ushindi ili kufikisha pointi 44 na kufufua matumaini yao ya kumaliza katika nafasi ya nne ambayo kwa sasa imekaliwa na Biashara United yenye alama 49 baada ya mechi 32.

Makocha wa timu zote mbili, Boniphace Mkwasa wa Ruvu  na Malale Hamsini wa Polisi wametamba kuingia kutafuta ushindi katika mchezo huo ili kuyasogelea malengo yao kwa msimu huu.

"Tunacheza nyumbani, tumejipanga kutumia vyema uwanja huu ili kupata ushindi ambao utatupunguzia presha ya kushuka daraja kwani tuna michezo migumu ambayo tunatakiwa kushinda yote," alisema Mkwasa.

Naye Malale alisema: "Tunatambua ubora  wa Ruvu lakini tunaenda kucheza mechi hii kwa nidhamu kubwa ili kuhakikisha tunapata matokeo yatakayoturudisha kwenye mbio za kuwania kumaliza ligi katika nafasi nne za juu," alisema.

Mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo ilikuwa Disemba 12, mwaka jana kwenye dimba la Ushirika mkoani Kilimanjaro Polisi wakiwa wenyeji na mechi kumalizika kwa suluhu (0-0).