Uko hapa: NyumbaniMichezo2022 01 15Article 585946

Soccer News of Saturday, 15 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Mabosi Yanga Waingilia Usajili Simba SC

Mabosi Yanga Waingilia Usajili Simba SC Mabosi Yanga Waingilia Usajili Simba SC

MABOSI wa Yanga Jumatano walikutana kujadili nafasi za kuzifanyia maboresho katika usajili wa dirisha dogo na kati ya hao ni nahodha na beki wa kati wa Biashara United, Abdulmajid Mangaro.

Mangaro ni kati ya mabeki waliopo katika mipango ya kusajiliwa na Simba.

Tetesi zilikuwa zinasema kuwa, Yanga ndiyo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kumsajili beki huyo, licha ya kuwepo katika mipango na Simba.

Mmoja wa mabosi wa Yanga, amesema kuwa bado timu hiyo ipo katika mazungumzo ya mwisho na Biashara ambayo inammiliki mchezaji huyo mwenye mkataba.

Bosi huyo alisema kuwa katika kikao hicho viongozi hao wamependekeza kufunga usajili na wachezaji wawili ambao ni beki ambaye ni Mangaro na winga mmoja mbadala wa Yacouba Songne atakayekuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima.

Aliongeza kuwa mabosi hao walitarajiwa kufanya kikao kingine leo (jana) jioni cha mwisho cha kuamua usajili wa Mangaro na winga huyo kabla dirisha kufungwa keshokutwa Jumamosi saa sita usiku.

“Viongozi wa Kamati ya Utendaji, Kamati ya Mashindano na Benchi la Ufundi la Yanga walikutana juzi (Jumatano) kujadili masuala mbalimbali ya timu na kikubwa kupitia ripoti ya Kombe la Mapinduzi na usajili.

“Katika usajili walijadili kuhusiana na kumsajili winga mwingine wa kigeni atakayekuwa mbadala wa Yacouba aliyepo nje ya uwanja akiuguza majeraha yake ya goti baada ya kufanyiwa oparesheni ambaye atakaa nje msimu mzima.

“Pia beki wa kati mmoja wa kigeni atakayekuwa mbadala wa Ninja (Haji Shaibu) aliyepelekwa nchini Tunisia kufanyiwa oparesheni ya goti na Mangaro ndiye anayetajwa kuchukua nafasi yake,” alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema: “Bado usajili haujafungwa, hivyo huenda tukasajili mchezaji yeyote na kikubwa tutafuata ripoti ya kocha wetu Nabi.”