Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 19Article 558265

Soccer News of Sunday, 19 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mahadhi ni mabao tu huko Geita Gold

Wachezaji wa Geita Gold wakishangilia baada ya Mahadhi kufunga goli Wachezaji wa Geita Gold wakishangilia baada ya Mahadhi kufunga goli

Kiungo mpya mshambuliaji wa Geita Gold, Juma Mahadhi ameendelea kukiwasha katika michezo ya kirafiki ya timu hiyo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Septemba 27, mwaka huu.

Mahadhi ambaye amejiunga na wachimba Dhahabu hao kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga ametupia mabao matatu katika mechi tatu alizoitumikia timu yake hadi sasa tangu alipojiunga nayo Agosti, mwaka huu.

Nyota huyo alifunga mabao mawili dhidi ya Kagera Sugar ugenini katika ushindi wa mabao 2-1 walioupata Septemba 12, mwaka huu kwenye mchezo wa kwanza wa kirafiki uliopigwa  dimba la Kaitaba mjini Bukoba.

Mahadhi ametupia tena leo kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya  dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo maalum wa Geita Gold Day uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita huku akishindwa kucheka na nyavu katika mchezo mmoja pekee waliotoka suluhu ya 0-0 dhidi ya Polisi Tanzania Septemba 16 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Nyota huyo ambaye alidumu Yanga kwa zaidi ya miaka mitano alikaa nje ya uwanja kwa mwaka mmoja na miezi tisa kabla ya kurejea mwaka jana na kupelekwa Ihefu kwa mkopo wa nusu msimu ambao aliumaliza na kutimkia Geita.

Akizungumzia maendeleo ya kikosi chake, Kocha Mkuu Ettienne Ndayiragije amesema anaridhishwa na juhudi za vijana wake ambao wamezidi kuimarika kila siku kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi huku akiwa na matumaini kuwa watakuwa fiti asilimia 100 na kuwa tayari kutoa ushindani pindi Ligi itakapoanza.

Geita Gold ambayo haijapoteza mchezo wowote wa kirafiki hadi sasa, itaianza Ligi Septemba 27 ugenini dhidi ya Namungo FC kwenye dimba la Majaliwa mjini Ruangwa kisha kuifuata Yanga Oktoba 2 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.