Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 16Article 557929

Habari za michezo of Thursday, 16 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mahakama yasubiri taarifa za Hansy Pope

Mahakama yasubiri taarifa za Hansy Pope Mahakama yasubiri taarifa za Hansy Pope

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, inasubiri taarifa rasmi ya kifo cha Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zacharia HansPope kufariki dunia.

Ni baada ya mawakili wa utetezi katika kesi inayowakabili viongozi watatu wa Klabu ya Simba, kuiomba Mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo, kutokana na mshtakiwa mmoja katika kesi hiyo kufariki dunia.

HansPope alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika hospitali ya Aga Khan, wakati akipatiwa matibabu baada ya kuugua ugonjwa wa Uviko-19 na mazishi yake yatafanyika Septemba 15, mkoani Iringa.

HansPope na wenzake wawili, aliyekuwa rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu, wanakabiliwa na mashtaka nane yakiweno ya kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha bila Kamati ya Utendaji ya Simba kukaa kikao.

Wakili wa washtakiwa hao, Benedict Ishabakaki na Kung’e Wabeya, walitoa taarifa hiyo, jana wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya Aveva kuendelea kujitetea, baada ya mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa wote.

Mawakili hao wakidai tarehe ijayo watawasilisha taarifa rasmi ya msiba wa HansPope ikiwemo cheti cha kifo.

“Mheshimiwa hakimu tunaomba kesi hii uiahirishe hadi tarehe nyingine kwa sababu tuna msiba, lakini tarehe ijayo tutakuja na taarifa rasmi ya msiba wa HansPope ikiwemo cheti cha kifo,” alidai Ishabakaki. Hakimu Mkazi Mkuu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo kupisha shughuli za mazishi.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 22, 2021 itakapoendelea.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Maghela Ndimbo, aliieleza Mahakama hiyo shauri hilo limeitwa mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kujitetea.

Hata hivyo, kutokana na sababu zilizotolewa na mawakili wa washtakiwa, Ndimbo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo.

Agosti 31, 2021 kesi hiyo ilishindwa kuendelea kutokana na HansPope kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani hapo kuhudhuria kesi yake. Hata hivyo, Jana Aveva na Nyange walikuwepo mahakamani hapo .

Katika shtaka la kughushi linalowakabili wote, inadaiwa tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya Dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh90 milioni huku wakijua sio kweli.

Pia katika mashtaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.