Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 10Article 556555

Habari za michezo of Friday, 10 September 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Makambo Awekewa Bil 1.5 awamalize Wanigeria

Makambo Awekewa Bil 1.5 awamalize Wanigeria Makambo Awekewa Bil 1.5 awamalize Wanigeria

JEURI ya fedha imeanza Yanga! Ndivyo utakavyoweza kusema baada ya uongozi wa timu hiyo kutangaza kwamba, endapo ushindi utapatikana nyumbani na ugenini katika mchezo Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United, basi wachezaji wao akiwemo mshambuliaji, Heritier Makambo watapewa bonasi ya shilingi bilioni 1.5.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Yanga itangaze Kamati Mpya ya Mashindano inayoongozwa na baadhi ya vigogo wakubwa wa klabu hiyo akiwemo Davis Mosha, Abdallah Bin Kleb, Seif Magali, Rogers Gumbo, Arafat Haji na Lucas Mashauri.

Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya kamati hiyo, ameliambia Spoti Xtra kuwa, matajiri hao wameweka bonasi ya Sh 500Mil kwa kila ushindi wa nyumbani.Bosi huyo alisema kuwa, ushindi wa ugenini wameweka Sh 1Bil kwa kuanzia mchezo wa Jumapili hii watakaocheza dhidi ya Rivers United kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo wakishinda zote, jumla wataondoka na bonasi ya Sh 1.5bil.

Aliongeza kuwa, kitita hicho cha bonasi kimewekwa kwa ajili ya kuongeza morali ya wachezaji ili kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kufika nusu au robo fainali ya michuano hiyo msimu wa 2021/22.

“Kama ilivyokuwa kauli mbiu yetu iliyotangazwa na Manara (Haji) ya The Return of Champions yenye maana kwamba mabingwa wamerejea, kikubwa tunataka kurejesha heshima ya klabu yetu iliyoptea.

“Hivyo ni lazima morali ya wachezaji iongezeke kwa kuhakikisha tunawapa mahitaji yao muhimu ikiwemo malazi, chakula na bonasi nzuri ili kufanikisha malengo yetu.

“Tunataka kufika hatua nzuri kama siyo kuchukua ubingwa wa Afrika, hivyo tumepanga kuwapa bonasi nzuri, kwa michezo yote ya nyumbani tutawapa wachezaji wetu Sh 500Mil na ugenini Sh 1Bil, hiyo ikitokea wakishinda,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kupitia Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alisema: “Kila mchezo wetu tunaoucheza wa mashindano kunakuwa na posho, hivyo katika michuano hii ya kimataifa kutakuwepo na bonasi ya wachezaji ambayo ni siri."