Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 03Article 555184

Habari za michezo of Friday, 3 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Makambo amshangaza Billo

Makambo amshangaza Billo Makambo amshangaza Billo

WAKATI straika Heritier Makambo akianza na makali yake ndani ya kikosi cha Yanga, moto wake umemshtua kocha Athuman Bilal ‘Billo’, aliyewaonya mabeki wa timu za Ligi Kuu akiwaambia jamaa karudi na utamu wake na kama hawatajipanga wataumizwa kama alivyofanya msimu wa 2017-2018.

Makambo, aliyerejea Jangwani Jumapili iliyopita kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi, alianza na moto kwa kufunga bao pekee wakati Yanga ikilala 2-1 na Zanaco kutoka Zambia kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Billo alisema mwanzoni alipata shaka kuona Makambo anarejeshwa Jangwani akihofia asiwe mwenye ubora na kiwango kama alichokuwa nacho awali, lakini kwa sasa ameuona mziki wake kwani amekuwa mtamu na kwamba straika huyo kutoka DR Congo ni yuleyule wa misimu miwili iliyopita.

Kocha huyo wa zamani Pan Africans, Stand United na Alliance alisema kwa jinsi alivyomuona kwa sasa kinachotakiwa ni kuhakikisha anapata mtu wa kumtengenezea mabao kwa kumlisha pasi za mwisho.

“Nilipata hofu kidogo kuona kama Makambo atakuwa bora kama yule aliyekuwa mwanzo na ndio maana nilimfatilia sana katika dakika zile alizocheza kwenye ule mchezo ni kweli bado yuko sawa kiwango chake kipo vilevile,” alisema.

Makambo aliondoka Yanga kujiunga na AC Horoya akiwa kinara wa mabao akifunga 17 na kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya kinara Meddie Kagere wa Simba aliyefunga 23.