Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 25Article 553621

Soccer News of Wednesday, 25 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mastaa Simba watakaokaa jukwaani

Kikosi cha Simba kikiwa Mazoezini, nchini Morocco walikokwenda kuweka Kambi Kikosi cha Simba kikiwa Mazoezini, nchini Morocco walikokwenda kuweka Kambi

Msimu unaoanza mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wamesajili wachezaji kumi, jambo ambalo halikutegemewa na wafuatiliaji wengi wa soka ndani na nje ya nchi kutokana na kiwango walichoonyesha msimu uliopita.

Katika kikosi cha Simba kulikuwa na mahitaji machache yaliyotakiwa kuzibwa. Ni wazi wimbi kubwa la wachezaji ambao Simba wamewasajili wengi wao kama sio kuishia benchi, basi watakuwa wale ambao wamesajiliwa muda mwingi kuishia jukwaani kuwa watazamaji.

JEREMIAH KISUBI

Miongoni mwa usajili ambao Simba wamefanya ni Jeremiah Kisubi waliyemtoa Tanzania Prisons waliyevutiwa naye kutokana na kiwango bora alichonyesha kwenye michezo ya Ligi Kuu.

Awali, Kisubi alikuwa anakwenda kumalizana na Yanga baada ya kukubaliana katika maeneo ya msingi, lakini Simba kama kawaida yao walimuwahi juu kwa juu na kumalizana naye licha ya kwamba mpaka wakati huu bado hawajamtambulisha.

Usajili huo wa Kisubi ni wazi, si rahisi kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa Aishi Manula amekuwa akionyesha hata katika mechi za kirafiki.

Hata msimu ujao ni wazi Manula atakuwa golini, jambo ambalo litamfanya Kisubi kuwa chaguo la pili au tatu kwani ushindani mwingine unaomsubiri ni dhidi ya Benno Kakolanya. Ukiachana na Manula na Kakolanya yupo pia Ally Salim ambaye alikuwa chaguo la tatu.

ISRAEL PATRICK MWENDA

Hakuna asiyefahamu uwezo wa beki wa kulia wa Simba, Shomary Kapombe ambaye amekuwa akicheza mara kwa mara kikosi cha kwanza.

Ubora wa kampombe ni pamoja na kushambulia, lakini kama haitoshi wamekuja wachezaji wengi wapya kwenye nafasi hiyo na kushindwa kufua dafumbele zake.

Israel Mwenda atakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kupata nafasi ya kucheza mbele ya Kapombe, kwani bila hivyo atakaa jukwaani au kuishia benchi kama ilivyokuwa kwa David Kameta ‘Duchu’ msimu uliopita.

HENOC INONGA

Katika mashindano ya ndani mabeki Joash Onyango na Pascal Wawa wameonyesha viwango bora na washambuliaji wa timu pinzani hupata wakati mgumu kupita mbele yao. Ubora huo utamuwia vigumu Henoc Baka kupata nafasi ya kucheza kama atashindwa kuonyesha kiwango bora zaidi ya pacha hiyo iliyocheza pamoja msimu uliopita.

Kama akishindwa kuonyesha makali mashindano ya ndani ni wazi atakuwa mchezaji wa kuishia jukwaani au benchi ila katika Ligi ya Mabingwa Afrika anaweza kucheza kwani Onyango na Wawa wamekuwa wakifanya makosa mengi.

Baka kama atashindwa kuwa bora atafuata nyayo za Peter Muduhwa msimu uliopita ambaye aliishia kusugua benchi na hatimaye kujikuta katika wakati mgumu tofauti na matarajio.

ABDULSAMAD KASSIM

Amesajiliwa na Simba kutokea Kagera Sugar ambayo chini ya kocha Mkenya Francis Baraza aliyetua katika kikosi hicho akitokea Biashara United hakuwa anamtumia mara kwa mara Kassim.

Katika nafasi ya kiungo mkabaji ambayo anacheza atakutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa viungo wanne wa Simba ambao hucheza mara kwa mara katika nafasi hiyo.

Kassim anatakiwa kukaza vya kutosha ili kupata nafasi ya kucheza, la sivyo atakuwa mchezaji wa kawaida na kuishia jukwaani kutokana na aina ya wachezaji ambao wanacheza katika eneo hilo

Katika nafasi ya kiungo mkabaji hutumika zaidi Mganda Taddeo Lwanga, huku Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni na Jonas Mkude katika vipindi tofauti wamekuwa wakipishana.

Ni wazi kama asipokaza Kassim kutokana na ushindani wa kutosha kutoka kwa Lwanga, Mzamiru, Mkude na Nyoni ambao ndio hutumika mara kwa mara, ataishia jukwaani.

JIMSON MWANUKE

Msimu uliomalizika akiwa na Gwambina FC alifanya vizuri kwa kufunga mabao pamoja na kutoa pasi za mwisho jambo ambalo liliwavutia Simba na kumsajili kwa mkataba wa miaka mitatu licha ya timu yake kushuka.

Mwanuke anacheza katika nafasi nne - zote za mbele ambazo katika kikosi cha Simba kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa na hutumika mara kwa mara kutokana na kufunga mabao muhimu, kutoa pasi za mwisho na msaada kwa timu.

Katika nafasi hizo za mbele mastraika mara nyingi huanza John Bocco, kinara wa mabao msimu uliopita na Chriss Mugalu aliyemaliza wa pili katika ufungaji msimu uliopita.

Ukiachana na mastraika hao wenye njaa ya mabao kuna Meddie Kagere ambaye licha ya kupata muda mchache wa kucheza amekuwa akifunga mabao ya maana kwa timu na kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa ligi mara mbili.

Wechezaji wengine ambao Mwanuke atakwenda kukutana nao katika kikosi hicho na walikuwa katika timu msimu uliopita ambao wanacheza kwenye safu ya ushambuliaji ni Rally Bwalya, Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga, Bernard Morrison na Said Ndemla.

SADiO KANOUTE

Kama Kanoute atakuwa katika

kiwango bora maana yake anaweza kuanza katika nafasi ya kiungo mshambuliaji na akianza na kiungo mmoja mkabaji ambaye anaweza kuwa Lwanga, Mkude, Mzamiru au Nyoni.

Kama akishindwa kuwa katika ubora maana yake Simba wataanza na viungo wawili wakabaji kati ya wanne walionao huku juu yao akicheza Bwalya kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.

Kanoute kazi itakuwa kwake kuwa mchezaji wa kuishia jukwaani au kwenda kuziba vizuri nafasi ya kiungo fundi Clatous Chama aliyetimkia RS Berkane ya Morocco.

KIBU DENIS

Kwa Kibu itakuwa kazi ngumu kupata nafasi ya kucheza mbele ya miamba mitatu - Bocco, Mugalu na Kagere ambaye msimu uliopita muda mwingi alikuwa akianzia benchi na kuingia kipindi cha pili au kutotumika kabisa.

Kibu ambaye alifanya vizuri msimu uliopita akiwa na kikosi cha Mbeya City mpaka kuwavutia Simba, anaweza kukutana na kivuli cha Charles Ilanfya aliyetoka KMC akiwa moto, lakini alishindwa kufanya vizuri na kurudi kwa mkopo timu hiyo.

Jambo kama hilo liliwakuta Adam Salamba, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza ambao wote walisajiliwa kwa matumaini makubwa kama Kibu kutokana na kufanya vizuri katika timu zao, lakini walipofika Simba walishindwa kufurukuta.

MAWINGA TISA

Katika kikosi cha Simba msimu uliopita ukiachana na Luis Miquissone na Chama ambao wameuzwa, wamebaki wachezaji wengine watano ambao wanacheza katika nafasi ya winga.

Wachezaji hao watano ambao msimu uliopita walicheza kama mawinga walikuwa Perfect Chikwende, Morrison,

Dilunga, Bwalya na Ajibu ambaye alijiondoa katika kikosi kabla ya kumaliza mechi za msimu na sasa yupo kamili.

Katika dirisha hili la usajili ambalo linaelekea ukingoni wamesajiliwa wachezaji wanne ambao wanaweza kucheza kama mawinga, na kati yao lazima wawili watacheza na wengine watakuwa benchi.

Mawinga ambao wamesajiliwa dirisha hili na itakuwa sio rahisi kwao kucheza kikosi cha kwanza iwapo hawatakaza msuli ni Peter Banda, Pape Sakho, Duncan Nyoni na Yusuph Mhilu. Kutokana na hali hiyo ni wazi usajili wa mawinga wanne na wale watano ambao walimaliza na kikosi msimu uliopita kuna wapya kwenye mechi nyingi wataishia benchi au kukaa jukwaani.