Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 10 02Article 560950

Soccer News of Saturday, 2 October 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mayele anataka mabao 15 tu Yanga

Mayele anataka mabao 15 tu Yanga Mayele anataka mabao 15 tu Yanga

SEPTEMBA 25, 2021 itabaki kwenye kumbukumbu ya wadau wa soka pale Fiston Mayele alipoifunga Simba dakika ya 11 tu tangu kuanza kwa mechi ya Ngao ya Jamii Uwanja wa Mkapa, bao ambalo lilipa ushindi Yanga na kutwaa tuzo hiyo.

Gazeti hili lilifanya mahojiano na Mayele ambaye alifunguka mambo mbalimbali ya ujio wake Yanga akitokea AS Vita ya DR Congo.

MAPOKEZI YANGA KIBOKO

Mayele anasema mapokezi Yanga yamemfanya ajisikie kama yupo nyumbani. “Ukianzia na mashabiki ambao walikuja uwanja wa ndege, pia viongozi wa timu, wachezaji wenzangu ilikuwa ni kama mtoto aliyesafiri na sasa anarudi nyumbani,” anaeleza Mayele ambaye msimu uliopita DR Congo alifunga mabao 12 nyuma ya mfungaji bora aliyetupia 13.

KUONDOKA AS VITA

Mchezaji huyo anasema aliondoka AS Vita ili kusaka changamoto katika mazingira mapya tofauti nyumbani.

“Watu wote wanajua kwamba Vita ni klabu kubwa yenye rekodi mbalimbali na imekuwa na ushiriki mzuri katika mashindano ya Afrika, lakini kuna wakati katika maisha unahitaji kitu na mazingira tofauti ya kazi, niliamua kuja Yanga nisaidie kuwainua ili nao wapate mafanikio zaidi,” anasema.

“Peke yangu sitaweza kukamilisha hilo, nimefurahi kuona uongozi unaonyesha kuwa na ndoto kubwa.”

ANAVYOIONA YANGA

Baada ya kutua Yanga kisha kukutana na wachezaji wenzake anakielezea kikosi hicho kwamba kimesheheni nyota wenye vipaji.

“Kwenye timu nimekutana na wachezaji wazuri ambao wana morali ya kutamani mafanikio, nafikiri hii ni sehemu sahihi,” anasema Mayele.

“Yanga ina wachezaji wazuri. Nilipofika na kuwaona nikajua natakiwa kufanya kazi kutokana na ushindani utakaokuwa mkubwa. Wanajua kucheza mpira watu kama Feisal (Salum), Kaseke (Deus), Yacouba (Sogne) na wengineo.”

AMEJIPANGAJE KUNG’ARA

Akiwa tayari ni kama ameanza kujihakikisha namnba kikosi cha kwanza, Mayele, hata hivyo ana jambo moja kubwa moyoni mwake.

“Kitu kizuri ni kujua malengo ya timu, lakini pia kama mchezaji kuwa na malengo yako umejiwekea. Klabu inataka kufanikiwa, lakini na mimi natakiwa kuweka nguvu ili kwa nafasi yangu kama mshamnbuliaji nifunge magoli mengi ambayo yataisaidia timu,” anasema.

“Najua natakiwa kushirikiana na wenzangu na kusikiliza kile ambacho makocha wanataka tukifanye katika kila mechi, siku zote nimekuwa nikitaka kuona kila mechi nakuwa na nguvu kubwa ya kufunga. Nataka hilo nilifanye na Yanga.”

MTAJI WA MABAO

Akizungumzia namna atakavyofanikiwa kutimiza malengo akiwa mshambuliaji kikosini, Mayele anasema ili straika afanye vizuri kuna aina ya huduma anayotaka akiwa uwanjani hasa kutoka kwa mawinga na viungo ambao muda aliokaa Yanga anasema watu hao wapo lakini kumbe alimsoma kitambo Feisal Salum ‘Fei Toto’.

“Yanga ina mawinga wazuri. Nilipokuwa Vita nilifunga sana, nilikuwa nacheza kwa ushirikiano mkubwa na Jesus (Moloko) na bahati kubwa naye amekuja hapa Yanga. Kitu kinachokuja sasa ni kuendeleza ile kazi nzuri tuliyofanya kule nyumbani. Pia wapo wengine kama kina Ambundo (Dickson) yupo Farid (Mussa).. hawa ni wachezaji wazuri.

“Katikati ya uwanja napo namuona Feisal, ni kiungo mzuri sana anajua kufanya kazi yake na kurahisisha kazi ya mshambuliaji. Namjua Feisal tangu nilipokuja hapa na timu ya taifa tukacheza na Tanzania. Ni mchezaji ambaye mshambuliaji yeyote angependa kucheza naye. Yuko pia Yacouba na Kaseke, hawa ni watu bora, najua kwamba kuna uhakika wa kupata pasi na hata mimi kuwapa pasi nao wakafunga,” anasema.

VIPI MOLOKO KWA KISINDA?

Kwa mashabiki wa Yanga alipouzwa winga Tuisila Kisinda kwenda RS Berkane ya Morocco, wengi hawakufurahi, lakini fasta viongozi wakamleta Moloko na hapa Mayele anawatofautisha akiwatuliza mashabiki

“Moloko ni mchezaji bora ambaye anajua kazi yake. Nimecheza naye na anajua kazi yake. Kama nilivyosema bahati nzuri kwangu niko naye pia hapa Yanga. Najua alikuwapo Tuisila, nilicheza naye Vita, ni winga mzuri. Pia nafurahi kuona ameuzwa ni heshima kwa klabu pia kule nyumbani wanaona alifanya kazi nzuri hapa.

“Yanga kumchukua Moloko ni kama Mungu amewapa mtu sahihi ambaye ametokea alikotokea Kisinda na alifanya kazi nzuri. Moloko atafanya kazi kubwa hapa na mashabiki watafurahi kama walivyofurahi kwa Kisinda. Sina wasiwasi kabisa wote wana kasi na wanajua kutengeneza nafasi.”

VIPI KUHUSU MAKAMBO?

Mayele ametua Yanga na kuungana na mshambuliaji mwingine, Heritier Makambo ambaye anatoka DR Congo na hapa anaeleza anavyomfahamu.

“Makambo ni ndugu yangu, tunatoka taifa moja. Nilikuwa namjua wakati fulani nyuma. Nilimuona anacheza pale Lupopo. Nimezaliwa Jiji la Lubumbashi na Lupopo iko hukohuko, ingawa hakucheza sana kule nyumbani, lakini namjua ni mshambuliaji mzuri. Nafurahi sasa tunatakiwa kufanya kazi pamoja hapa na nilichoshtuka anapendwa sana na mashabiki wa Yanga. Hii inaonyesha kwamba alifanya kazi nzuri na mimi inanifundisha watu wa Yanga kama ukiwafanyia kazi nzuri utabaki katika mioyo yao,” anasema.

MABAO 15

Baada ya kufunga mabao 12 akiwa na AS Vita katika msimu wake wa mwisho, anasema lengo lake Yanga ni kuo-ngeza idadi hiyo angalau afunge mabao 15 msimu huu. “Kitu kibaya kwa mshambuliaji ni kutofunga, sitarajii hilo kama linaweza kunitokea, ila naamini msimu huu utakuwa mzuri kutokana na aina ya wachezaji ambao wanaunda hii timu na kisha tukacheza pamoja,” anasema.

“Nikiwa Vita nimewahi kuwa mfungaji bora mara mbili, lakini mara ya mwisho nimefunga mabao 12. Ningetamani kuona naongeza kidogo mabao hayo nikiwa hapa Yanga nataka mabao 14 au 15. Naamini sitakuwa nimefanya vibaya katika msimu wa kwanza.”

SIRI JEZI NAMBA 9

Kila klabu ina utamaduni wake na ndani ya Yanga jezi namba 9 imekuwa kama na gundu kwani hakuna aliyewahi kuivaa kisha akafanya vizuri, lakini Mayele fasta ameitaka hatua ambayo iliwashtua baadhi ya watu.

“Hii ni namba ambayo nimekuwa nikiitumia kwa muda mrefu sana na hakuna timu ambayo nimekwenda nikaikosa. Nilifurahi kuikuta pia hapa. Unajua familia yetu kuna watu wanane sasa mimi huwa napenda kutumia ile 9 ili nione kama tuko watu 9 kila sehemu ambayo naenda,” anasema.

WAKONGOMANI SITA YANGA

Msimu huu Yanga ina Wakongomani sita kikosini ambapo baadhi ya watu wanaamini sio sahihi kuwa nao wengi kiasi hicho, lakini Mayele mtazamo tofauti.

“Kwanza ni furaha kuona mnakutana na watu ambao mnatoka taifa moja, sijaona kama kuna ubaya jambo zuri kwetu ni kama linatupa presha ya kutakiwa kuonyesha kazi nzuri Yanga.

Itaendelea kesho