Uko hapa: NyumbaniMichezo2022 01 09Article 584512

Soccer News of Sunday, 9 January 2022

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Miezi miwili ya Pablo Simba, kuna mwanga au bado giza ?

Pablo Franco Martin Pablo Franco Martin

Kocha Pablo Franco Martin ametimiza miezi miwili tangu alipojiunga na Simba akitokea timu ya Al Qadsiah ya Kuwait ambayo alikuwa akiinoa hapo kabla.

Ndani ya muda huo ambao Pablo Franco ameiongoza Simba kuna mafanikio ya haraka ya nje na ndani ya uwaja ambayo imeyapata lakini yapo ambayo anapaswa kuyafanyia kazi siku za usoni kutokana na udhaifu ambao Simba imeonyesha

Makala hii inaangaza yale ambayo Simba imenufaika nayo chini ya Pablo katika siku 60 alizoiongoza lakini pia yale ambayo inapaswa kurudi katika ubao na kuhakikisha inayatibu.

MAFANIKIO

Hapana shaka Wanasimba wengi kwa sasa wana imani kubwa na Pablo kutokana na mazuri mengi aliyoyafanya ndani ya timu hiyo.

Licha ya kupewa timu ikiwa katika wakati mgumu, kocha huyo amefanya mambo yafuatayo.

KURUDISHA MABAO

Katika mechi nane za mashindano ambazo Pablo ameiongoza Simba ndani ya muda huo wa miezi miwili, timu hiyo imeonekana kuwa tishio katika kufumania nyavu tofauti na ilivyokuwa katika mechi nane kabla yake.

Jumla ya mabao 16 yamefungwa na Simba katika michezo nane iliyoongozwa na Pablo ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo wakati kabla yake, timu hiyo ilifunga mabao sita tu katika mechi nane ambayo ni wastani wa bao 0.75 kwa mechi.

SOKA LA KUVUTIA

Mwanzoni mwa msimu huu, Simba sio tu haikuwa ikifunga mabao mengi bali pia haikuwa inacheza aina ya soka lake la pasi ambalo liliifanya itengeneze nafasi nyingi za mabao katika msimu uliopita.

Timu hiyo ilikuwa inatumia zaidi mipira ya juu jambo ambalo lilifanya iwe rahisi kudhibitiwa na wapinzani lakini mambo yamekuja kuwa tofauti mara baada ya ujio wa Franco.

Kocha huyo amerudisha staili ya Simba ya kucheza soka la kuvutia na jambo kubwa zaidi ameifanya icheze kwa kasi na hivyo kuifanya iwaweke wapinzani katika wakati mgumu tofauti na hapo mwanzo.

NAFASI KWA WACHEZAJI, KUPANDISHA MORARI

Simba chini ya uongozi wa Pablo imetoa nafasi ya kucheza kwa idadi kubwa ya wachezaji tofauti na watangulizi wake ambao walikuwa hawawachezeshi baadhi ya wachezaji.

Kocha huyo Mhispania amejitahidi kutoa nafasi kwa kila mmoja na kujipa muda wa kumtaza na nimchezaji mmoja tu wa ndani ambaye hajacheza chini yake na wengine ni wa nafasi ya ukipa ambayo ni nadra kocha kubadili wachezaji mara kwa mara.

Mchezaji pekee wa ndani ambaye hajacheza chini ya Pablo ni Abdulswamad Kassim aliyetolewa kwa mkopo katika dirisha hili dogo la usajili lakini kiungo huyo pia hata kwa makocha waliopita hakucheza.

Kitendo cha kujaribu kutoa nafasi kwa kila mchezaji kumechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha hali ya kujiamini kwa wengi wao na angalau sasa timu hiyo inaonekana kuchangamka.

KUIMARIKA KWA NIDHAMU YA TIMU

Siku chache kabla ya ujio wa Pablo, nidhamu ndani ya kikosi cha Simba ilionekana kushuka na ilionekana makocha kukosa utawala mbele ya wachezaji.

Ilifika hatua hadi wachezaji walikuwa wanaingilia majukumu ya benchi la ufundi pindi mechi zilipokuwa zinaendelea lakini mambo yamebadilika chini ya Pablo.

Mhispania huyo ameweza kurudisha nidhamu ya timu na sasa benchi la ufundi linaheshimika tofauti na hapo awali.

ALIPOCHEMKA

Pamoja na kazi kubwa aliyoifanya, kocha Pablo anaonekana ameshindwa kuifanya Simba iwe na safu imara ya ulinzi na chini yake imekuwa ikiruhusu mabao mara kwa mara tofauti na hapo awali ambapo ilionekana kuwa ngumu kufungika.

Katika mechi nane za kwanza za msimu huu kabla ya ujio wa Franco, Simba iliruhusu mabao manne tu ikiwa ni wastani wabao 0.5 kwa mchezo lakini katika mechi nane za kwanza za Pablo, timu hiyo imeruhusu jumla ya mabao sita ikiwa ni wastani wa bao 0.75 kwa mchezo.

WADAU WAFUNGUKA

Nyota wa zamani wa Simba, Musa Hassan Mgosi anasema kuwa timu hiyo imeonyesha mabadiliko makubwa chini ya Franco.

“Timu kwa sasa imerudi katika ule ubora wake na wachezaji wanaonekana wanafurahia kile wanachokifanya na inapata matokeo mazuri hivyo pongezi kwa kocha ameibadilisha kiukweli,” anasema Mgosi.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ anasema kuwa wana imani kubwa na kocha huyo na mafanikio wanayopata uwanjani ni ishara tosha ya ubora wa Pablo.