Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 26Article 553804

Soccer News of Thursday, 26 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Miguu ya Mdamu inavuja damu Dar

Mathius Mdamu (aliyelala) akiwa hospitali Mathius Mdamu (aliyelala) akiwa hospitali

Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba miguu ya staa wa Polisi Tanzania, Mathius Mdamu inavuja damu kwenye vitanda vya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Mdamu alipata ajali Julai 9 wakiwa wanatoka mazoezini katika Uwanja wa TPC wakirejea kambini kuelekea mechi za mwisho za msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuvunjika miguu yote miwili.

Mwanaspoti ambalo limekuwa likiripoti habari za mchezaji huyo tangu siku ya kwanza alipoumia, lilimshuhudia pia jana mchana akiwa kitandani Muhimbili huku viongozi wengi wa timu yake wakikwepa kuzungumzia hali yake.

Ilimtumia Mdamu kama dakika tano kushusha pumzi na kuzungumza na Mwanaspoti, huku uso wake ukiwa umejaa machozi yaliyoambatana na maneno ya uchungu, akiomba Mungu amsikie kama anavyowasikia wengine ili anyanyuke kitandani.

Mwanaspoti lilimtembelea Mdamu, aliyelazwa Taasisi ya Mifupa ya MOI ili kumjulia hali yake lakini ukweli mchungu ni kwamba hali yake ni mbaya na anahitaji msaada wa hali na mali kuokoa maisha yake kwani hata mkewe mwenye mtoto mdogo alionekana mwingi wa mawazo.

Katika mazungumzo yake ameanza kwa kusema “Ujumbe wangu naupeleka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu, nimempoteza mama yangu nikiwa mdogo sana, nafarijika kuona wewe unaongoza nchi ni mama, naomba uniangalie kwa jicho la mama na mwanae.”

“Natamani ningepata bahati kama wanayopata wengine ambao mama umewatembelea, ili uone miguu yangu ilivyo naamini ungefanya kitu cha kuongeza nguvu mimi kwenda kutibiwa nje kwa wakati kabla mambo hayajaendelea kuwa mabaya zaidi,” Baada ya kumaliza kutamka hayo ameangua kilio huku miguu yake ikiwa na vidonda vibichi vinavyohitaji ujasiri kuvitazama.

Hali ya huzuni ikatawala huku mke wake akiwa pembeni yake, akishindwa kujizuia machozi.