Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 04Article 540997

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Minziro avizia Simba, Yanga

MABOSI wa Geita Gold iliyopanda Ligi Kuu Bara wamemhakikishia Fred Felix Minziro kuendelea kukinoa kikosi hicho na fasta kocha huyo mwenye zali lake amesema atafanya usajili wa wachezaji 15 wakiwamo mastaa kutoka Simba na Yanga ili kujiimarisha kwa msimu wao kwanza wa ligi.

Uongozi wa Geita umesisitiza utaendelea kufanya kazi na Minziro, lakini wataboresha benchi lao la ufundi ili kuhakikisha timu yao inakuwa kali na yenye ushindani katika msimu wao wa kwanza wa kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

Minziro, aliyeipaisha Geita kutoka Daraja la Kwanza (FDL) akirejea rekodi yake aliyoifanya kwa Singida United na KMC, aliliambia Mwanaspoti kuwa, amepanga kusajili nyota hao wakiwamo watakaoachwa Simba na Yanga, lakini wenye viwango vizuri ili kutumia uzoefu wao kuwabeba.

Kocha huyo aliyeiwezesha pia Geita kuwa Mabingwa wa FDL kwa kuitungua Mbeya Kwanza kwa bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa jijini Dar es Salaam, alisema ili kupata timu yenye ushindani, lazima aboreshe kikosi chake kutokana na ukweli Ligi Kuu Bara ni ngumu.

“Ligi Kuu ni ngumu sana, hatutaki kuja kushiriki tunakuja kushindana, mimi naangalia wachezaji watakaokuwa na msaada katika timu, hata kama watatoka Simba na Yanga, ilimradi wawe na uwezo na kuipigania timu ili iwe na ushindani kwelikweli,” alisema Minziro aliyeongeza kuwa, hana wasiwasi wala shaka na kanuni mpya za makocha kusimamia timu kuwa na Leseni B na kusema kuwa yeye ni mkongwe na hana shaka na hilo kwa kuwa anayo Leseni ya Daraja A.

Naye Katibu wa Geita Gold, Revinus Ntare alisema hawajapanda daraja kwa kuba-hatisha, ili walipambana na kufika hapo walipo na wanajipanga kuhakikisha hawarudi nyuma kwani wanataka kuifanya timu yao iwe na ushindani katika msimu wao wa kwanza Ligi Kuu Bara.

“Tutasajili wachezaji wapya 15 watakaoungana na 10 walioipandisha na niwatoe hofu mashabiki wetu, kocha Minziro tutaendelea kuwa naye, japo tutaboresha benchi la ufundi na tayari tumeshaanza mazungumzo na wachezaji wengi kwa sasa,” alisema Ntare.

Join our Newsletter