Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 15Article 551656

Soccer News of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mitihani mitano mapro wapya Simba, Yanga

Miongoni mwa Wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga Miongoni mwa Wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga

Msimu uliopita wa 2020/2021, Simba ilionekana kuwa na mafanikio zaidi kwa timu za Bongo ikibeba kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilimaliza nafasi ya pili kwenye ligi, lakini ikaambulia kubeba Kombe la Mapinduzi pekee na hivyo kuendelea na jinamizi baya la kukosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu minne mfululizo.

Sasa tunaelekea katika msimu mpya ambao mashabiki watakwenda kushuhudia mabadiliko kwenye timu hizo mbili kubwa nchini ambazo zimesajili wachezaji wengi wapya wakiwemo raia wa kigeni.

Simba imeuza nyota wake wawili muhimu, kiungo Clatous Chama aliyetimkia RS Berkane ya Morocco na Luis Miquissone ambaye ameuzwa kwa mabingwa wa Afrika, Al Ahly ya Misri, wakati Yanga imempiga bei winga Tuisila Kisinda katika timu ya RS Berkane, huku pia ikiwaacha wachezaji wake wengi wa kigeni waliokuwa na timu hiyo msimu uliopita.

Sasa hii ni mitihani mitano watakayokutana nayo wachezaji wapya wa Simba na Yanga ambayo wanapaswa kupambana kufaulu, kwani kama wakishindwa basi wajiandae kisaikolojia kukutana na zomeazomea kutoka kwa mashabiki wa klabu hizo.

KUONGEZA USHINDANI

Jambo la kwanza analotakiwa kufanya mchezaji akisajiliwa ni kuisaidia timu yake kufikia malengo. Katika soka malengo hayafikiwi bila kuwa na ushindani chanya wa hali ya juu, hivyo wachezaji wapya wanatakiwa kufanya mtihani huu na kuufaulu. Ushindani huu haupaswi kuishia kwenye mechi za ndani tu, bali hadi kimataifa kwani malengo makuu ya Simba, Yanga na Azam ni kufanya vizuri katika mashindano ya hayo makubwa.

KUZIBA PENGO

Simba imewaachia Miquissone na Chama wakati Yanga haitakuwa na Kisinda na wengine ambao waliongeza ladha na burudani ndani ya vikosi hivyo msimu uliopita.

Je wachezaji wapya wataweza kuziba mapengo yao? Sio rahisi. Inahitajika juhudi za hali ya juu kujitoa na kufanya vitu ambavyo havitawakumbusha mashabiki uwepo wa kina Chama, Miquissone na Kisinda. Huu ni mtihani wa pili ambao nyota wapya wanapaswa kuujibu kupitia miguu yao.

KUONGEZA MVUTO

Hakuna anayebisha kuwa msimu uliomalizika Ligi Kuu ilikuwa na mvuto mkubwa, jambo lililowashawishi watu wengi kwenda kuangalia mpira uwanjani na wengine kutazama kwenye runinga. Pamoja na mambo mengine, lakini mvuto zaidi uliletwa na soka safi lililokuwa likipigwa na wachezaji ndani ya uwanja.

Watu walienda uwanjani kutaka kuona namna Kisinda anavyowakimbiza mabeki na wengine walifuata pasi za ‘upendo’ za Chama ilhali wapo waliotaka kuona chenga za maudhi za Miquissone. Je wapya watakuja na nini cha kuongeza mvuto zaidi na kufanya ligi inoge zaidi? Kazi wanayo.

KUKUZA LIGI

Katika misimu minne iliyopita Ligi Kuu Bara imepiga hatua kubwa. Ipo katika ligi 10 bora za Afrika na hadi sasa ina nafasi nne za uwakilishi wa timu kwenye michuano mikubwa ya soka barani Afrika kwa ngazi ya klabu.

Mafaniko hayo hayajaja kwa bahati mbaya, bali yametokana na ushindani, ubora wa timu na wachezaji ambao ndio wahusika wakuu uwanjani.

Wachezaji wapya hususan wa Simba, Yanga na Azam wanahitaji kuendeleza walipokuta na sio kuirudisha nyuma wala kuifanya ibaki ilipo. Huu ni mtihani mwingine mgumu kwao.

KUBURUDISHA

Unaweza kuona kuburudisha sio jambo muhimu sana kwenye soka, lakini inabidi uamini kuwa ni burudani ya pekee. Unajua mashabiki tofauti na kuzisapoti timu zao wanafuata nini uwanjani? Wengi hufuata burudani.

Ubora wa wachezaji pamoja na vituko mbalimbali vya ndani na nje ya uwanja ndizo burudani kubwa ambazo mashabiki wengi wa soka wanapenda kuona.

Wachezaji wapya wanapaswa kuwa wabunifu ndani ya uwanja ili kutoa burudani kwa mashabiki kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengi wa Simba na Yanga walionogesha ligi msimu uliopita.

Mastaa mbalimbali katika Ligi Kuu msimu uliopita wakiongozwa na Chama ambaye kiwango chake kilikuwa burudani tosha kwa mashabiki sio wa Simba tu bali hata wapinzani wao wakubwa Yanga, walilifanya soka litazamike na kushangiliwa viwanjani.

Wachezaji wengine walioleta burudani kwenye ligi msimu uliopita ni Mukoko Tonombe wa Yanga aliyekuwa na staili yake ya kushangilia kama mwalimu anayefundisha wanafunzi, Benard Morrison, Pascal Wawa, Erasto Nyoni na Ibrahim Ajibu wa Simba ambao hawakuishiwa vituko ndani na nje ya uwanja na kugeuka vivutio kwa mashabiki wa soka nchini.