Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 11Article 556864

Habari za michezo of Saturday, 11 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Msigwa Aeleza Alivyowasiliana na Hans Pope Kabla ya Kifo

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa (kushoto), kulia ni Marehemu Hans Pope Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa (kushoto), kulia ni Marehemu Hans Pope

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Maelezo, Gerson Msigwa amepokea kwa masikitiko nmakubwa kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zakaria Hans Pope ambaye amefariki dunia Ijumaa ya jana, majira ya usiku katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.

Msigwa amewapa pole Simba na kusema mara ya mwisho aliwasiliana na Zakaria kupitia simu kwa njia ya ujumbe mfupi ambapo alimweleza namna alivyokuwa akiugua na kupatiwa matibabu.

"Nimeshtushwa sana na kifo cha Zacharia HansPope. Tumepoteza mdau muhimu kwa soka la nchi yetu na mtu aliyetamani kuona Tanzania inakaa kwenye viwango vya kimataifa vya soka.

"Poleni sana wanafamilia, uongozi wa Simba SC wachezaji, wapenzi na wanachama wa Simba wapenzi wa soka na wote walioguswa na msiba huu (wa Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Simba, Zakaria Hanspope).

"Mara ya mwisho niliwasiliana nae (Hanspope) kwa kuchati nikimpa pole kwa maradhi yanayomkabili, alinijibu huku akiwa kwenye mashine ya oksijeni (mashine ya kumsaidia kupumua). Aliniambia “ugonjwa unatesa sana huu” na baadaye akasisitiza watu wachukue tahadhari.

"Tumuombee (Zakaria Hanspope) apumzike mahali pema, tuwaombee wafiwa na tumuenzi kwa kuendeleza dhamira kubwa aliyekuwa nayo katika kuendeleza soka la Tanzania. Mungu amweke mahali pema peponi, Amina," amesema Msigwa.