Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 23Article 543844

Habari za michezo of Wednesday, 23 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwigulu: Simba ilistahili ubingwa Afrika 2020/21

Mwigulu: Simba ilistahili ubingwa Afrika 2020/21 Mwigulu: Simba ilistahili ubingwa Afrika 2020/21

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameipongeza Simba kwa ubora ilioonesha msimu huu, akisema ilistahili kuchukua ubingwa wa Afrika.

Akizungumza bungeni Dodoma, Dk Nchemba amesema kilichowagharimu Simba kutolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kukosa mipango.

“Niipongeze Simba imepiga hatua kubwa sana mwaka huu, lakini nilivyokuwa naingalia ilikuwa inaenda kuchukua ubingwa,” alisema na kuongeza kuwa Wekundu hao wa Masimbazi walifungwa Afrika Kusini kwasababu hawakuwa na mipango.

Katika mechi ya kwanza ya hatua ya robo fainali, Simba ilifungwa mabao 4-0 na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kabla ya kushinda nyumbani Dar es Salaam mabao 3-0 lakini hayakutosha kuwavusha.

“Kwenye michezo bado tunakosa mipango, kuna mahali tumekosea hasa pale ambapo hatuweki vipaumbele, yaani kwetu sisi mambo yote yako sawa tu.”

“Haipendezi kama timu ina mchezo muhimu wa kimataifa halafu katikati kunakuwa na mchezo wa watani wa jadi kwani hata Simba inaonekana iliwekeza nguvu zake zote kwenye mchezo dhidi ya Yanga ambao baadae ulisogezwa mbele na ilipoenda Afrika Kusini haikuwa na mipango mizuri,” alisema.

Dk Mwigulu alisema lawama za Simba kuwanyooshea vidole watani zao na mshauri wa Yanga, Senzo Mazingisa kwamba waliwahujumu kufungwa na Kaizer Chiefs ni za bure, anachoamini kuna michezo walikosa mipango.

“Simba ilienda kucheza Afrika Kusini bila mipango ya mchezo, yenyewe ilijiandaa na mechi ya mtani na mimi niwapongeze Yanga walivyoenda uwanjani wakakaa dakika kadhaa wakaona wenzao hawapo wakajua wanajiandaa na mchezo huo,” alisema.

Alisema timu zinazokwenda kwenye mashindano ya kimataifa zinaleta sifa kwa taifa hivyo ni muhimu Bodi ya Ligi izipe kipaumbele na kutoingiza michezo ya watani.

“Niwapongeze Wanayanga ambao waliiunga mkono Simba,” alisema huku akiingiza utani kuwa, wameiunga mkono Simba kwa kuwapa Bernard Morrison licha ya wekundu hao kuwa na mashabiki wenye heshima hawakuwahi kurudisha tiketi ya kuletwa mchezaji huyo.

Mwigulu ni shabiki wa Yanga na amewahi kuwa kwenye kamati kadhaa za klabu hiyo.

“Wanayanga muendelee na upendo huo na waachieni tu Morrison anakuja Makambo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewateua mshambuliaji wa kimataifa anayecheza soka la kulipwa Uturuki, Mbwana Samatta, msanii na mwanamitindo, Hamisa Mobeto na mchambuzi wa soka Edo Kumwembe kuwa mabalozi wa kuhamasisha ulipaji wa kodi.