Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 23Article 559243

Soccer News of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Nabi Awaondoa Hofu Yanga

Kocha wa Yanga, Nabi. Kocha wa Yanga, Nabi.

Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kutamka kuwa wapo imara, tayari amewatengeneza kisaikolojia nyota wake ili kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Simba.

Timu hizo kongwe Jumamosi hii saa kujmi na moja kamili zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Katika mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani ikiwa na uchungu wa kutoka kutolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria.

Nabi alisema kuwa watarejea uwanjani wakiwa imara huku wakiwa na uhakika wa kuwatumia nyota wao watatu muhimu katika michuano ya kimataifa ambao ni Fiston Mayele, Shaban Djuma na Khalid Aucho ambao ITC zao zilichelewa kufika.

Nabi alisema anaamini nyota hao wataongeza nguvu katika kikosi chake atakachokitumia katika mchezo huo unaosubiriwa na mashabiki wa timu hizo mbili pinzani.

Aliongeza kuwa, anatarajia kuingia uwanjani kivingine kwa kubadili mfumo na mbinu za uchezaji kutokana na uwepo wa nyota hao wa kimataifa waliokosekana katika Caf.

“Nafahamu mashabiki wamechukizwa na kutolewa Caf, hivyo kama kocha nina kibarua kigumu cha kuhakikisha ninarejesha furaha ya mashabiki kwa ushindi.

“Kikubwa ninachokifanya hivi ni kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji wangu wote kwa kuwasahaulisha matokeo ya michuano ya kimataifa na badala yake kuelekeza nguvu zetu katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

“Mashabiki wa Yanga watarajie mabadiliko ya kikosi changu, mfumo na mbinu kutokana na uwepo wa wachezaji wangu Djuma, Mayele na Aucho ambao hatukuwatumia katika Caf baada ya ITC zao kuchelewa.

“Uwepo wa wachezaji wetu hao kutaongeza nguvu na kuwafunga wapinzani wetu Simba, naendelea kukiboresha kikosi changu katika baadhi ya maeneo ili kuhakikisha tunarejesha furaha ya mashabiki,” alisema Nabi.