Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 24Article 559537

Soccer News of Friday, 24 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Nabi: Simba Tunawafunga

Kocha Nabi wa Yanga Kocha Nabi wa Yanga

KUELEKEA mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaopigwa kesho Jumamosi, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amefunguka kuwa kwa maandalizi ambayo kikosi chake kimeyafanya, ana imani kubwa wataifunga Simba, huku akiwapa kazi maalum washambuliaji wake Heritier Makambo na Fiston Mayele.

Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, kuanzia saa 11:00 jioni ambapo Simba ndio watakuwa wenyeji.

Hii itakuwa mara ya nne kwa Yanga na Simba kukutana ndani ya mwaka huu, ambapo katika michezo mitatu iliyopita, Yanga imeshinda mbili, fainali ya Kombe la Mapinduzi na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, huku Simba wakishinda fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Akizungumza maandalizi ya mchezo dhidi ya Simba, Nabi alisema, baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika, nguvu zao wamezihamishia michuano ya ndani.

“Tumefunga ukurasa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, tunafungua ukurasa mwingine, mechi dhidi ya Simba ni kubwa, tunajiandaa na tutajituma ili tupate ushindi. “Kwanza ninawaheshimu wapinzani wangu, lakini itakuwa mechi ambayo lazima mmoja ashinde, hatuwezi kupoteza hiyo mechi kwani maandalizi ni mazuri, morali ipo juu, timu itacheza kwa kujituma.” alisema Nabi na kuongeza.

“Suala la safu ya ushambuliaji tunalifanyia kazi, kuna namba kubwa ya wachezaji wa nafasi hiyo akiwemo Makambo, Mayele na Yusuph, kwa maandalizi ambayo tunawapa hilo tatizo litaisha na tunaamini hata mechi ya Jumamosi tutafunga mabao kulingana na aina ya wachezaji tulionao.