Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 21Article 558865

Habari za michezo of Tuesday, 21 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Nabi amtaja Mayele, Djuma Simba, Yanga

Kocha Mkuu wa Yanga, Prof Nabi Kocha Mkuu wa Yanga, Prof Nabi

Yanga juzi ikiwa ugenini nchini Nigeria, ilikubali tena kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Rivers United kama ilivyokuwa wiki moja iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, hivyo kutolewa kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-0.

Hivyo, kwa sasa Yanga ambayo imerejea nchini jana ikitokea Nigeria, inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, mchezo ambao utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi ukiwa ni maalum kwa ajili ya kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2021/22.

Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kufurushwa nje ya michuano hiyo ya CAF, Nabi alisema mchezo huo umepita na sasa anaumulika ulio mbele yao dhidi ya Simba Jumamosi ambao anaamini utakuwa mgumu.

"Kuhusu mechi ya Jumamosi, itakuwa tofauti kwa kuwa nitakuwa na maingizo mengine kama Djuma [Shabani], Mayele [Fiston], ambao wanaruhusiwa kucheza mechi hiyo, hivyo wataongeza nguvu katika kikosi," alisema.

Kwa upande wa sababu ya kutolewa mapema katika michuano hiyo ya CAF, Nabi alisema kubwa ni kutokuwa na maandalizi mazuri ya mwanzo wa msimu 'pre season', lakini wakikabiliwa na matatizo mengi ya baadhi ya wachezaji kukosa vibali, pamoja na kuathiriwa kisaikolojia na wapinzani wao kuwasingizia baadhi ya wachezaji wao kuwa wana maambukizi wa ugonjwa wa COVID-19.

Nabi alisema sababu kubwa ya kwanza ni kikosi kutokuwa na maandalizi mazuri ya msimu ambayo yamesababisha kutokuwa na stamina na pumzi, hasa kipindi cha pili.

"Kipindi cha kwanza tulicheza vizuri sana, tatizo pekee lilikuwa ni kufunga magoli. Kipindi cha pili nguvu ilipungua, hatukuwa na pumzi na stamina ilikuwa ndogo na haya yamesababishwa na kutopata maandalizi ya kutosha ya msimu.

"Pili ni kwamba wapinzani wetu walitutoa kwenye mchezo, baada ya kutuambia kuwa kuna baadhi ya wachezaji wana maambukizo ya corona, hii ilitufanya kutuondoa kwenye mchezo, kwani hata walivyokubali, lakini tayari kisaikolojia walikuwa wametuathiri," alisema kocha Nabi.

Kocha huyo pia ameeleza pia sababu nyingine ni kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake tegemeo ambao alitarajia wangekuwa sehemu ya kikosi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hawakuwapo kutokana na kukosa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Wachezaji hao ni Mayele, Djuma na Khalid Aucho.

"Kwa hiyo hapo utaona kuwa timu ilikuwa ina bahati mbaya, ilikuwa inakabiliwa na matatizo mengi, lakini kwa sasa naangalia mechi inayofuata ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na wachezaji hao watakuwapo," alisema.