Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 19Article 572692

Soccer News of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Nabi atawashangaza Simba

Nasredinne Nabi Nasredinne Nabi

Yanga inapiga hesabu ndefu itachukuaje pointi 6 za ugenini kabla ya kukutana na Simba, lakini kabla ya kuanza safari kuna mabadiliko makubwa wakayafanya ambayo lazima yawashtue wapinzani wao katika mechi za Ligi Kuu Bara ikiwamo Kariakoo Derby iliyipangwa kupigwa Desemba 11.

Kama hujui ni kwamba, wikiendi hii yaani Jumamosi Yanga itakuwa pale Uwanja wa Ilulu, mjini Lindi wakiwa wageni wa Namungo na baada ya hapo watatua jijini Mbeya kuwafuata wazee wa ‘comeback’ Mbeya Kwanza.

Wakimaliza mechi hizo akili zote zitakaa sawa na kurejea Dar es Salaam kupambana na Simba ya Kocha Pablo Franco na sasa mambo yakaanzia hapo kubadilika, kwani Kocha Nasreddine Nabi amepanga kufanya sapraizi bab’kubwa katika pambano hilo la 107 katika Ligi ya Bara tangu 1965.

Kocha Nabi ameliambia Mwanaspoti kuwa, watakuwa na mabadiliko ya mbinu zao kuelekea mchezo huo wa watani waliowatungua katika mechi ya Ngao ya Jamii.

Wakongwe hao watavaana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi yao ya kwanza ya Ligi msimu huu, huku Simba ikiwa haijaonja ushindi wowote dhidi ya Yanga, tangu iliposhinda mara ya mwisho Feb 16, 2019 kwa bao la Meddie Kagere.

Nabi alithibitisha, hata sura ya kikosi chake itakuwa imebadilika kuanzia mechi ya wikiendi hii dhidi ya Namungo na ile ya Mbeya kabla ya kuvaana na Simba, huku akiwasisitiza mastaa wake juu ya umuhimu wa kucheza kwa umakini.

“Kutakuwa na mabadiliko ya kikosi hilo ni uhakika tunatakiwa kuwa kamilifu zaidi katika mechi hizo, tukianzia na hii ya Namungo tayari nimezungumza na wachezaji watakaopata nafasi kupambana kwa nia ya kuendeleza rekodi nzuri ya timu,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tunatakiwa kuwa makini kila mchezo, kwani ni kama fainali, nimewaambia wachezaji hakuna mechi rahisi tunatakiwa kushinda kwa ubora wa mbinu zetu. Tunatakiwa kumaliza mechi hizo za mkoani, kisha tujipange dhidi ya Simba.”

Wakati Nabi akijipanga hivyo uongozi nao ukashusha mabadiliko ya ghafla juu ya safari yao ya kuifuata Namungo.

Yanga awali ilipanga kuondoka jijini Dar es Salaam jana, lakini ghafla mambo yamebadilishwa, japo inafanya siri juu ya safari hiyo, lakini Mwanaspoti linajua timu hiyo itaondoka leo kwenda Lindi, ikipishana saa chache na Simba iliyoondoka jana jioni kwenda jijini Mwanza.

Simba itavaana na Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba katika pambano la Ligi Kuu Bara likipewa jina la ‘El Clasico ya Bongo’, Ruvu ikijipabitiza jina la Barcelona kwa aina ya soka inalopiga, huku Simba ikinasibishwa na Real baada ya kuajiri walioinoa, Pablo Franco na De Castro.