Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 23Article 553243

Soccer News of Monday, 23 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nabi awatumia shushushu Wanigeria

Kocha Mkuu wa Yanga,  Nasreddine Nabi Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi

Yangaa inahesabu siku tu kabla ya kukutana na Rivers United ya Nigeria katika mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa mwezi ujao, lakini kocha wao Nesreddine Nabi fasta amefanya jambo ili kuhakikisha wanatoboa mbele ya wapinzani wao hao.

Unaambiwa Nabi anawapigia hesabu wapinzani wao hao na sasa ameshaanza kazi ya kujua makali yao.

Yanga itaanzia nyumbani dhidi ya Rivers mchezo ambao huenda ukapigwa Septemba 12 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kisha kurudiana baada ya wiki moja nchini Nigeria na hesabu mapema zikaanza.

Kocha Nabi amepata taarifa kwamba wapinzani wake hao wako nchini Benin wakicheza mashindano flani mafupi ya kujiweka sawa yanayoshirikisha timu kama tano hivi kutoka mataifa matano tofauti.

Alichofanya Nabi ameangalia ratiba yake na kugundua ugumu wa kufika nchini Benin lakini fasta akamsaka mtu anayemuamini ili aweze kumpa kila taarifa ya ubora wa Rivers.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Nabi amesema anajua kila kitu juu ya uwepo wa Rivers nchini Benin na kwamba tayari amempa kazi rafiki yake mmoja mwenye ujuzi wa kuisoma timu ili aweze kumpa taarifa za kutosha.

Nabi amesema wakati anatafuta taarifa hizo anajipanga kuhakikisha timu yake inapata maandalizi ya kutosha kujiandaa na mechi hizo mbili za mtoano.

“Tunawafuatilia, najua kwamba kuna mashindano kule Benin wanacheza, tayari kuna mtu nataka aende akafuatilie kujua kipi kinaendelea katika timu yao, hatutakiwi kudharau mpinzani,” amesema Nabi.