Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 02 21Article 525688

Soccer News of Sunday, 21 February 2021

Chanzo: habarileo.co.tz

Namungo karata muhimu leo

Namungo karata muhimu leo Namungo karata muhimu leo

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Namungo wanatarajiwa kushuka uwanjani kuikabili Primeiro de Agosto ya Angola kwenye mchezo wa mtoano kusaka nafasi ya kuingia hatua ya makundi leo.

Mchezo huo awali ulikuwa uchezwe Angola na warudiane Dar es Salaam lakini kutokana na mapokezi mabaya waliyopata Namungo mchezo huo ulifutwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na sasa yote itachezwa katika Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo huo ni muhimu kwa Namungo kupambana kuhakikisha inashinda mchezo huo wa kwanza na ule wa marudiano utakaochezwa Februari 25, mwaka huu ili kusonga mbele hatua inayofuata.

Namungo ilifika hatua hiyo baada ya awali kuzitoa Al Rabita ya Sudan Kusini na El Hilal Obeid ya Sudan.

Mchezo wa kwanza na Al Rabita walishinda mabao 3-0 na wa pili ulifutwa baada ya Shirikisho la Soka nchini Sudan Kusini (SSFA) kushindwa kukamilisha taratibu za waamuzi waliopangwa kuchezesha mechi hiyo.

Mchezo wa mzungumko wa pili dhidi ya El Hilal Obeid walishinda wa kwanza kwa mabao 2-0 na wa pili wakatoka sare ya mabao 3-3.

Wapinzani wao Primeiro waliangukia hatua hiyo wakitoka Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walipoteza mchezo dhidi ya Kaizer Chief baada ya kwanza kufungwa bao 1-0 nyumbani na ule wa ugenini walitoka suluhu.

Mwenendo wa Namungo sio mzuri hasa kwenye ligi ya nyumbani ila wanapokuja kwenye michuano hiyo mikubwa wamekuwa wakifanya vizuri.

Namungo ina nafasi kama itatumia mazingira ya nyumbani kufanya vizuri katika michezo yote miwili na kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele hatua ya makundi.

Kocha Mkuu Hemed Morocco alisema wamejipanga kupambana na lengo lao ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kuingia kwenye makundi.

“Tumedhamiria kushinda mchezo huo na maandalizi yetu yako vizuri, kikubwa ni kupambana kwa uwezo wetu ili kutimiza tulichokusudia. Tunajua Primeiro ni moja ya timu nzuri Angola na zenye uzoefu ila hatuhofii tunachotaka ni ushindi,”alisema.

Primeiro ni timu ya jeshi la Angola yenye uzoefu na michuano hiyo na ndio mabingwa wa nchi hiyo.

Waliwahi kufika nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018 na katika Kombe la Shirikisho waliwahi kufika hatua ya robo fainali mwaka 2009.

Join our Newsletter