Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 20Article 552592

Soccer News of Friday, 20 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ndayiragije huyoo Geita Gold

Etienne Ndayiragije Etienne Ndayiragije

Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Etienne Ndayiragije amerejea tena nchini na anatarajia kukinoa kikosi cha Geita Gold kilichopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Ndayiragije ni mzoefu wa Ligi Kuu Bara baada ya kuwahi kuzinoa Mbao, KMC na Azam kwa nyakati tofauti.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Geita Gold kililiambia gazeti hili kuwa timu hiyo iko katika mazungumzo ya mwisho na kocha huyo Mrundi kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho ambacho kwa sasa kinanolewa na Fred Minziro.

“Kocha tayari ameshawasili nchini kwa ajili ya kukamilisha makubaliano, lakini hatuwezi kutangaza kwa sasa mpaka pale mambo yatakapokuwa yamekamilika,” kimesema chanzo hicho.

Alipotafutwa mwenyekiti wa Geita Gold, George Mbiligenda alisema ni kweli hawana kocha mkuu wa timu baada Minziro kumaliza mkataba wake, lakini bado wapo kwenye mazungumzo naye.

“Minziro ni kocha mzuri kaipambania timu na kuipandisha Ligi Kuu msimu huu, lakini mkataba wake umemalizika na tupo kwenye mazungumzo naye sambamba na makocha wengine ambao tunaona wanaweza wakawa chachu ya mafanikio kwa timu yetu,” amesema Mbiligenda.

Kama Geita itafanikiwa kumnasa Ndayiragije itakuwa jambo baya kwa Minziro ambaye amekuwa na rekodi ya kuzipandisha timu Ligi Kuu kisha kisha humtema.

Minziro amewahi kuzipandisha KMC na Singida United kisha timu hizo kuamua kuachana naye na kuajiri makocha wengine.