Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 05 26Article 539908

Habari za michezo of Wednesday, 26 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Maajabu Yanga, kanuni na Kamati ya Saa 72

Maajabu Yanga, kanuni na Kamati ya Saa 72 Maajabu Yanga, kanuni na Kamati ya Saa 72

BILA shaka umeshawahi kusikia Yanga Kampuni na Yanga Asili. Lakini utakuwa umewahi kusikia kuhusu Yanga Katiba na Yanga Ukuta. Hayo ni makundi yaliyowahi kuibuka ndani ya Yanga katika nyakati tofauti kutokana na malumbano na migogoro iliyosababishwa na siasa za ndani ya klabu hiyo kongwe.

Miaka kadhaa baada ya hali kutulia na kumalizika kwa zama za migogoro kama ile ambayo mara zote iliishia kwenye mapinduzi, sasa vinaibuka vitu vidogovidogo ambavyo kimsingi vinawavunjia hadhi viongozi wa klabu hiyo. Mojawapo ni hili la kanuni ambalo liliwafanya watoe timu uwanjani siku ya mechi dhidi ya Simba.

Yanga walisema kanuni za ligi zilikiukwa, hivyo hawapo tayari kuruhusu ukiukwaji wa kanuni. Mashabiki wao waliwaelewa na baadhi ya watu, hasa wanaojiita wachambuzi ambao hawaijui vizuri historia ya Yanga na kiapo chao cha ‘Bishana hadi ufe’, waliwatetea sana kwamba walikuwa sahihi.

Mara zote nilipopata nafasi ya kulizungumzia hilo kwenye visiwa vyetu vya kahawa, nilisema wazi kwamba Yanga waliwaogopa Simba. Nasema kwa kujiamini kabisa kwamba Yanga hawakutoka uwanjani kwa ajili ya kulinda kanuni, walitoka kwa ajili ya kuogopa kichapo cha aibu kwa sababu hawakuwa na imani na timu yao, kanuni ilikuwa kichaka tu cha kujifichia. Nasema kwa sababu mechi iliyofuata baada ya hapo, Yanga walipigwa faini na Kamati ya Saa 72 iliyo chini ya Bodi ya Ligi kutokana na kukiuka kanuni kwenye mchezo wao dhidi ya Namungo. Yanga walituhumiwa kuingia uwanjani kwa kutumia geti la mashabiki na kuvunja kanuni ya 15(1) ya Ligi Kuu.

Haiingii akilini kwamba walichagua kulinda kanuni dhidi ya Simba tu, lakini hawakutaka kulinda kanuni dhidi ya Namungo. Kichaka cha kanuni ambacho wamekitumia leo, kinafanana na kile cha makubaliano walichokitumia mwaka 2008 kwenye Kombe la Kagame, walikataa kucheza na Simba kutafuta mshindi wa tatu.

Safari ile, Yanga walisema walikubaliana na Simba wagome, lakini Simba wakawasaliti. Hata hivyo, ukweli ni kwamba Yanga walikuwa na majeruhi sita wa kikosi cha kwanza ambacho kilicheza nusu fainali na kutolewa.

Hadi mechi dhidi ya Simba inafika, wachezaji wale muhimu walikuwa hawajapona, wakaona isiwe tabu, wakatunga uongo wa makubaliano, wakakimbia. Safari ile makubaliano, safari hii kanuni, Yanga ni ile ile!

MAAJABU KAMATI SAA 72

Mei 18, mwaka huu, Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Kuu maarufu kama Kamati ya Saa 72, ilitoa taarifa ya kikao chao cha Mei 17 na kuainisha hukumu kadhaa zikiwemo za watumishi watatu wa Azam FC. Watumishi hao ambao wamefungiwa miezi miwili, walituhumiwa kufanya makosa Mei 15, kwenye mchezo wao dhidi ya KMC.

Mzee wa Upupu anashangaa kuona kamati hii imeweza kutumia muda pungufu wa saa 72 kuwahukumu watu hawa, ilhali kuna kesi zilikaa hadi miezi mitatu bila kutolewa uamuzi na kamati hiyohiyo.

Leo hii kamati hii pendwa inaweza kukaa na kutoa uamuzi chini ya saa 72, ni maendeleo makubwa sana haya. Ni haya maendeleo ambayo mimi nayaita maajabu. Tangu lini Kamati ya Saa 72 ikakaa na kutoa hukumu mapema kiasi hicho?

Mtu unaweza ukadhani kwamba yawezekana kulikuwa na mpango maalumu dhidi ya Azam FC. Watumishi waliofungiwa walikuwa na hatia ya kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kistaarabu mwamuzi. Lakini, mwamuzi wa mchezo ule, Nadim Mohamed, anasema hakuona mashambulizi yoyote dhidi yake na wala hakuandika taarifa yoyote kuhusiana na hilo, sasa hii kamati imeyatoa wapi hayo madudu?

Hata hivyo, kitu kikubwa hapa ni kwamba kamati imekaa mapema sana na kutoa maamuzi. Tunataka mwedelezo wa hili, mara zote kamati ikae mapema namna hii na kufanya uamuzi, hii itasaidia sana kutoa haki kwa wanaostahili ili mpira wetu upige hatua.

Mojawapo ya mambo yanayoturudisha nyuma ni kuchelewa kusikilizwa kwa baadhi ya mashauri, hivyo kuharibu mipango ya wengine. Kamati imefanya vizuri, tunaipongeza, lakini hata hivyo ihakikishe inakuwa na mwendelezo wa hili na itende haki zaidi.