Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 21Article 573151

Habari za michezo of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Pablo: 'Tumecheza vizuri lakini mambo bado'

Pablo: Mambo bado Pablo: Mambo bado

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema licha ya ushindi wa mabao 3-1 iliopata timu yake dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu, bado ana kazi kubwa ya kufanya ili iweze kuendelea kushinda na kupata matokeo mazuri.

Pablo alisema hayo Mwanza juzi baada ya mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba. “Timu yangu ilicheza vizuri hasa kipindi cha kwanza na lengo letu lilifanikiwa. wachezaji pia walikuwa na morali hivyo nimechukua mapungufu na nitayafanyia kazi,’’ alisema Pablo.

Alisema watatumia wiki ijayo kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 28. Alisema mchezaji Bernard Morrison kucheza katika nafasi ya kiungo ilikuwa ni sehemu ya mipango yake na aliamua kufanya hivyo kutokana kuchelewa kurejea kwa wachezaji Rally Bwalya na Peter Banda.

Aliwapongeza wachezaji kwa mchezo mzuri na kiwango kizuri licha ya kuwa walikosa penalti katika kipindi cha pili. Naye Kocha Msaidizi wa Ruvu Shooting, Mohamed Nakuchema alisema hawakutegemea matokeo hayo na Simba iliwazidi katika kila idara. Katika msimamo wa ligi, Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza michezo sita na kushinda minne na sare mbili na kufunga mabao sita na kufungwa bao moja.

Ruvu Shooting ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi sita, imeshinda mechi mbili dhidi ya Coastal Union na Biashara United na imepoteza mechi nne dhidi ya Yanga, Simba, Polisi Tanzania na Dodoma Jiji. Wakati huo huo, Simba leo inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa Mwaka kwa mujibu wa katiba katika ukumbi wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na ajenda zimetumwa kwa wanachama, huku akiwataka kufika kwa wakati. “Mkutano utaanza saa 3:00 asubuhi hivyo wanachama wafike kwa wakati ili wajadili na kupitisha yale yote ambayo yatawasilishwa kwa mujibu wa katiba,” alisema.